Bashe azindua kiwanda cha pamba cha Chato

14Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Chato
Nipashe
Bashe azindua kiwanda cha pamba cha Chato

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amezidua Kiwanda cha Pamba cha Chato (CCU) na kuielezea hatua kama mpango kabambe wa serikali wa kujenga sekta ya kilimo inayojitegemea sambamba na uhakika wa upatikanaji wa
malighafi.

Akizungumza  baada ya kukizindua mwishoni mwa wiki, Waziri Bashe alisema kufufuliwa kwa kiwanda hicho mwanzo mzuri kwa wakulima pamba kuongoza uzalishaji na kuinua vipato vyao.

“Mradi wa kufufua kiwanda hiki umegharimu jumla ya Sh. 6,714,804,447 kutoka katika benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), lengo likiwa kuimarisha sekta ya kilimo ili kuwanufaisha wakulima wa pamba,’’ alisema Bashe.

Alisema kufufuliwa kwa kiwanda hicho ambacho kilisimama kufanyauzalishaji kwa miaka kadhaa kutawafanya wakulima wilayani Chato na maeneo mengine ya jirani kuongeza uzalishaji, hivyo kuleta unafuu wa maisha kwa wakulima.

“Serikali imedhamiria kuifanya sekta ya kilimo inajitegemee kwa kuwa mbali ya kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi, pia imekuwa na mchango wa asilimia 25 katika pato la Taifa,’’ alisema.

Aidha, waziri Bashe aliipongeza benki hiyo kwa jitihada zake za kuwaletea wakulima maendeleo kwa kuwapa mikopo yenye masharti nafuu jambo ambalo linaongeza tija katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, alisema kuzinduliwa kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la pamba ambayo ilishuka tangu msimu wa 2013/14.

“Tunaamini hatua tunazochukua kwa mazao ya kimkakati ikiwamo zao la pamba iyasaidie katika kuongeza thamani yake na hivyo kuwa na bei ambayo itamfanya mkulima anufaike zaidi na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa,” alisema.

Alisema bei ya msimu huu imekuwa nzuri ukilinganisha na misimu kadhaa ya hapo awali, na kwamba wataendelea kuimarisha upatikanaji wa soko zuri na lenye faida kwa mkulima.

Kiwanda hicho kitanufaisha Vyama vya Ushirika wa kilimo na Masoko (AMCOS) 52 vyenye jumla ya wakulima 7,000 kutoka Chato, Biharamulo na Muleba.

Habari Kubwa