Bei ya petroli, dizeli, mafuta taa zaongezeka

07Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bei ya petroli, dizeli, mafuta taa zaongezeka

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza ongezeko la bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yanayoingia Tanzania.

Mabadiliko hayo ya bei ya mafuta kwa wanunuzi wa jumla na rejareja inayoanza kutumika leo Jumatano Aprili 7, 2021 yametokana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, bei za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh142 na Sh85 kwa lita, huku bei ya jumla ikiongezeka kwa Sh141.92 na Sh84.95 kwa lita, mtawaliwa Ongezeko la bei hizo linamaanisha kuwa sasa wakazi wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,123 na dizeli kwa Sh1,996 kutoka Sh1,981 na Sh1,911 waliyokuwa wakinunua mwezi uliopita.

Mabadiliko ya bei hizo pia yamegusa mikoa ya Kaskazini yaani Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh73 na Sh105 kwa lita.

Pia bei ya jumla ya petroli na dizeli ikiongezeka kwa Sh72.38 na Sh105.12 huku bei ya mafuta ya taa ikiendelea kusalia kama ilivyokuwa katika toleo la Machi 3, 2021.

Hiyo ikiwa na maana kuwa wakazi wa Arusha watanunua lita moja ya petroli na dizeli kwa Sh2,211 na Sh2,081 ikilinganishwa na Sh2,139 na Sh1,975 waliyonunulia mwezi uliopita.

Mikoa ya Kusini, Mtwara, Lindi na Ruvuma bei ya rejareja ya petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh92 na Sh200 mtawalia.

“Kufuatia mabadiliko hayo kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura.”

“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika,” inaeleza taarifa ya Ewura.

 

Habari Kubwa