Bei ya sukari bado tatizo wanaouza rejareja

22May 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Bei ya sukari bado tatizo wanaouza rejareja

LICHA ya serikali kufanikiwa kuwadhibiti wafanyabiashara wakubwa wa sukari katika uuzaji wa bidhaa hiyo, bado kumekuwa na changamoto kwa wafanyabiashara wa rejareja kutekeleza bei elekezi kwa Mkoa wa Dodoma ya Sh. 2,900 kwa kilo.

Bei ya sukari kwa wafanyabiashara wa rejareja kilo moja wanauza kwa Sh. 3,000 tofauti na bei iyotangazwa na serikali kuwa katika mkoa wa Dodoma wananchi wauziwe kwa Sh. 2,900.

Mmoja wa wasambazaji wa sukari mkoani hapa Salman Gullamal, akizungumza jijini hapa jana, alisema hakuna sababu ya wafanyabiashara wa sukari kuuza bidhaa hiyo zaidi ya bei elekezi kwa kuwa wamewapunguzia bei ya bidhaa hiyo.

Alisema mfuko wa kilo 50, za sukari anauza Sh. 130,000 kutoka bei ya awali ya Sh. 137,000, alisema kwa mfanyabiashara wa rejareja ana uwezo wa kuuza kilo moja Sh. 2,700 na akapata faida.

“Nashindwa kuelezwa shida ni nini hadi bei ya sukari bado inakuwa kubwa kwa wauzaji wa rejareja ambao wanawahudumia wananchi, bei ninayowauzia hapa wana uwezo wa kuwauzia wananchi hadi Sh. 2,700 na wakapata faida, tunatakiwa kupata faida kidogo ili tusimkandamize mlaji,” alisema Gullamal.

Mkazi wa Dodoma, Fideles Timothy, alisema wanashangazwa na kitendo cha kuuziwa sukari kilo moja kwa Sh. 3,000 hadi 5,000 na ameiomba serikali kuwachukulia hatua wafanyabiashara wa aina hiyo.

Hata hivyo, aliiomba serikali kuharakisha kufikishwa bidhaa hiyo waliyotangaza kwamba imeingia nchini ambayo anadai kuwa itapunguza makali bei ilivyo sasa.

Mfanyabiashara wa sukari kwa bei ya rejareja, Antonia Kessy, alisema kinachosababisha kuuza bidhaa hiyo zaidi ya Sh. 3,000 ni kuongezekana gharama za ufanyaji wa biashara.

Alisema sio wote wana usafiri wa kusafirishia bidhaa hizo bali wanakodi kwa ajili ya kuchukulia mzigo huo.

Habari Kubwa