JPM afagiliwa kufungua utalii

20May 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
JPM afagiliwa kufungua utalii

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli, kwa uamuzi wake wa kutaka baadhi ya shughuli muhimu za maendeleo ikiwamo sekta ya utalii kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya kukuza uchumi na pato la wananchi.

Mwakilishi wa Jimbo la Amani, Rashid Ali Juma, alisema kauli za  Magufuli zimewatia moyo wananchi wengi na sekta muhimu ya utalii kwa kutaka kuona kwamba shughuli hizo zinarudi katika siku za hivi karibuni kwa sababu janga la ugonjwa wa corona limeanza kudhibitiwa.

Juma alisema hayo wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa mwaka wa fedha 2020-2021 katika Baraza la Wawakilishi.

Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi ambayo imeathirika vibaya katika sekta ya utalii, ambayo huingiza fedha za kigeni kwa asilimia 80 kutokana na kusitishwa kwa shughuli za uingizaji wa wageni.

“Naunga mkono kauli ya Rais Magufuli ya kurudisha shughuli za utalii ikiwamo kuingia kwa ndege zitakazobeba wageni kwa sababu kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa corona...na sisi kwa upande wetu tunatakiwa kuanza kufanya maandalizi ya aina hiyo,” alisema.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Konde, Omar Seif Abeid, alisema wakati umefika sasa kwa kamisheni ya utalii kujiweka sawa kwa maandalizi ya kuanza kufanya mawasiliano ya safari za watalii kuja nchini.

Alisema ugonjwa wa corona usitumike kusitisha shughuli za maendeleo na kukuza uchumi, ambapo cha msingi ni kuchukua kila aina ya tahadhari kupambana na ugonjwa huo.

''Nimefurahishwa na hotuba ya Rais Magufuli yenye kutoa moyo ya kuwajenga kimawazo Watanzania kujipanga kufanya shughuli zetu za maendeleo na kiuchumi, hivyo ugonjwa wa corona  usitumike kukwamisha mikakati ya maendeleo,” alisema.

Naye Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, aliipongeza Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa kufanya kazi kubwa ya kuinuwa sekta ya utalii ya ukarabati wa majengo ya kale pamoja na magofu.

Alisema utalii wa mambo ya kale ndio utaivusha Zanzibar katika miaka ijayo kwa kuwawezesha watalii wenye hadhi kuja na kuona historia ya mambo ya kale.

“Nimefurahishwa na mikakati ya wizara katika malengo ya kuimarisha utalii wa mambo ya kale yakiwamo magofu ambayo hutumiwa na watu mbalimbali kujua historia ya mambo ya kale na watawala wake,” alisema.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alipotembelea eneo la Hospitali ya Rufani eneo la Binguni Wilaya ya Kati Unguja, alisema serikali inakusudia kuanza kupunguza masharti ya ugonjwa wa corona, ikiwamo kufungua shule baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.