Kairuki apigia debe uwekezaji mkonge

07Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
MWANGA
Nipashe
Kairuki apigia debe uwekezaji mkonge

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angellah Kairuki, amewataka wananchi kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na mamlaka za serikali za mitaa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuwekeza katika tasnia ya mkonge, ambayo imeonekana kuwa na chachu kubwa ya maendeleo.

Kairuki alitoa rai hiyo baada ya kutembelea shamba la mkonge la Kisangara, lililoko chini ya kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL), Mwanga mkoani Kilimanjaro na kupewa taarifa ya upungufu wa mashine kwa ajili ya kuchakata zao hilo.

Alisema wananchi wanaweza kujiunga katika vikundi kama ambavyo imekuwa ikielekezwa na halmashauri na kupewa mkopo ambao watauwekeza katika ununuzi wa mashine ya kuchakatia mkonge, maarufu kama corona na kupiga hatua kimaendeleo.

“Nimeelezwa kuwa kuna upungufu wa mashine za kuchakata mkonge, hivyo wakati mwingine mkonge upo ila hakuna mashine ya kuchakata. Sasa viongozi wa halmashauri na hata mkoa, tuendelee kuwahamasisha wananchi wawekeze katika zao la mkonge, ambako kumeonekana kuwa na fursa nzuri,” alisema Kairuki.

“Tunaweza pia kutumia fursa ile ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuona ni namna gani kikundi cha pamoja au vikundi vya ushirika vinaweza kuwekeza katika ununuzi wa mashine ya kuchakatia mkonge.  Wananchi wachangamkie fursa hii ili kumaliza tatizo la upungufu wa mashine hizi,” aliongeza.

Waziri Kairuki alitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa halmashauri kutoa elimu kwa wananchi na kuelezea fursa zilizopo katika mkonge ili kupanua wigo wa uwekezaji katika kilimo hicho kwa kuwa mahitaji ya mkonge bado ni makubwa nchini na hata duniani.

“Mahitaji ya mkonge bado ni makubwa, hivyo tuendelee kuhamasisha wananchi na kuwapa elimu ili wale wenye maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho, wawekeze huko. Lakini pia tunaendelea kukaribisha wawekezaji wengine kuingia katika uchakataji wa zao hili,” alisema.

Kairuki alibainisha kuwa kwa sasa kuna viwanda 11 vikubwa na vya kati na viwanda vidogo zaidi ya 70 kwa ajili ya uchakataji wa zao hilo.

Awali, Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kanda ya Kaskazini, Daudi Riganda, aliutaka uongozi wa shamba hilo kuongeza uzalishaji na kuwekeza zaidi katika zao hilo ili kutengeneza faida.

“Bado hatujaridhika na namna ambavyo mwekezaji ametumia fursa ya uwekezaji katika kilimo hiki cha mkonge ikilinganishwa na rasilimali ya ardhi aliyonayo pamoja na hali ya hali ya hewa iliyopo. Ningeshauri wawekezaji watakaopewa nafasi ya kuwekeza katika kilimo cha mkonge, waongeze uzalishaji na kuwekeza kwa tija zaidi,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, alisema kwa sasa wanajipanga kutoa elimu na kuhamasisha wananchi, kujiingiza katika kilimo cha mkonge ili kuboresha maisha yao kwa kutumia fursa zilizopo nchini.

Habari Kubwa