Sababu ndege za Tanzania kupeleka mazao ya bustani nje

29Jun 2020
Ashton Balaigwa
Mbeya
Nipashe
Sababu ndege za Tanzania kupeleka mazao ya bustani nje

SERIKALI imekusudia kuuza mazao ya bustani yakiwamo ya mboga, viungo na matunda katika nchi za Asia na Ulaya kwa kuyasafirisha kwa kutumia ndege zake mpya ilizozinunua hivi karibuni.

Hatua hiyo inatokana na mazao hayo kuhitajika katika masoko ya nchi hizo, huku ikitarajia kujenga soko kubwa jijini Dar es Salaam ili chai inayozalishwa nchini inunuliwe na mataifa mengine.

Lengo la maamuzi hayo ya serikali ni kupambana na ujanjaujanja unaofanyika katika soko nchini Kenya, ambapo baadhi ya matunda na mboga yanayozalishwa nchini yanapelekwa nchini humo kuuzwa nje ya nchi na kuonekana yamezalishwa humo. Mazao hayo ni pamoja na  parachichi na chai inayouzwa katika masoko ya Mombasa na Nairobi.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa na Waziri wa Kilimo, Japhet Husunga, wakati akizindua maonyesho ya kilimo biashara yanayofanyika katika mashamba darasa ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI-Uyole) iliyopo mkoani Mbeya yenye lengo la kuwabadilisha wakulima kutoka katika kilimo cha kujikimu ili kulima kilimo biashara pamoja na kuzungumza na watafiti wa taasisi hiyo.

“Mwaka jana sisi wenye eneo kubwa katika sekta ya bustani tumepata dola milioni 779 wakati Kenya kwenye sekta hiyo wamepata zaidi ya dola bilioni 6 wanatumia ujanja wa maparachichi yetu kuchukuliwa na kupelekwa Kenya, wanaenda kuuza nje kwa kuweka lebo ya Kenya… sasa tunataka kukomesha ujanja huo tunaanza kupeleka wenyewe kwenye masoko hayo ya Ulaya na Asia kwa kutumia ndege zetu,” alisema Hasunga.

Mazao  ya mboga na matunda yatasaidia kuongezea Taifa fedha za kigeni zitakazotokana na kilimo hicho baada ya kupungua fedha hizo zilizokuwa zikiingia kutokana na utalii kufuatia ugonjwa wa COVID-19 ulioikumba dunia.

Hasunga alisema kuwa mojawapo ya mikakati mingine ya kuingiza serikali fedha za kigeni ni kupitia kilimo na kujenga soko kubwa la chai katika Jiji la Dar es Salaam ili chai inayozalishwa nchini iuzwe hapa.

Alisema ili kufikia mikakati hiyo, serikali imeanza mpango wa kuongezea TARI fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuzalisha mbegu bora za kisasa na zenye tija na kuongeza uzalishaji wa mazao hayo yatakayoiingizia Taifa fedha za kigeni ili yaweze kuzalishwa kwa wingi nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo, alisema kuwa wapo tayari kuzalisha mbegu mama za mazao hayo ya bustani, mboga na matunda kwa kuvitumia vituo 17 vya taasisi hiyo ya kilimo Tanzania kwa lengo la kusaidia serikali kuingiza fedha za kigeni.

Alisema TARI imekuwa ikizalisha mbegu teknolojia ya kisasa ya mazao ya mafuta ikiwamo zao la michikichi, alizeti na karanga kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini na hivi karibuni imepewa jukumu jipya la kuzalisha mbegu za zao la mkonge kwa kutumia vituo vyake vya utafiti na zinafanya vizuri katika uzalishaji.

Akizungumzia maonyesho hayo ya kilimo biashara, Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Uyole, Dk. Tulole Bucheyeki, alisema yamelenga kuzifikisha teknolojia mpya zilizofanyiwa utafiti moja kwa moja kwa wakulima ili kuachana na kilimo cha kujikimu na kulima kibiashara.

Alisema hatua hiyo inatokana na nchi hivi sasa kuelekea katika uchumi wa viwanda hivyo malighafi kubwa itakayohitajika inatokana na mazao yanayotokana na kilimo, hivyo wameamua kuanza kuwaandaa wakulima kulima kwa kutumia mbegu zenye teknolojia ya kisasa ambazo zinaongeza tija kwa mkulima na kuwa na uhakika wa uzalishaji.

Mmoja wa wakulima ambaye amehudhuria maonyesho hayo, Shukuru Mwakibete, alisema kwa kupitia maonyesho hayo ameweza kujifunza mbinu mbalimbali katika kilimo cha viazi mviringo kwa kutumia mbegu za teknolojia za kisasa ambalo limekuwa ni la kibiashara hasa kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya.

Habari Kubwa