Tamwa yaasa wajasiriamali kutokata tamaa

04Jun 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Tamwa yaasa wajasiriamali kutokata tamaa

MKURUGENZI wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), upande wa Zanzibar, Dk. Mzuri Issa, amewataka wajasiriamali kutokata tamaa licha ya changamoto katika harakati zao za uzalishaji wa bidhaa.

MKURUGENZI wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), upande wa Zanzibar, Dk. Mzuri Issa:PICHA NA MTANDAO

Dk. Mzuri aliyasema hayo wakati wa ziara maalumu ya kutembelea vikundi katika shehia mbalimbali za Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kujionea namna wajasiriamali wanavyofanyia kazi elimu wanayopewa kupitia chama hicho.

Aliwataka wajasiriamali hao kutokata tamaa licha ya changamoto walizonazo ikiwamo ya ukosefu wa huduma ya maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Alisema kuna jitihada kubwa zimefanywa na wajasiriamali na wanapaswa kuungwa mkono kwa kuwa lengo lao ni kujikwamua na umaskini.

Pia, alisema Tamwa-Zanzibar itaendelea kufanya kila jitihada zenye lengo la kuhakikisha wanawasaidia wajasiriamali hao ili waweze kutimiza ndoto zao.

Katika hatua nyingine aliwataka wanawake kuzitumia fursa mbalimbali kwenye jamii ikiwamo za kushiriki katika harakati za uchaguzi kugombea nafasi za kisiasa.

Aliwataka wanawake hao kuacha kubweteka na kudhani nafasi za uongozi ni za wanaume pekee badala yake wanapaswa kujitambua na kuwa tayari muda wowote.

Naye ofisa uwezeshaji wanawake kiuchumi Tamwa-Zanzibar, Nairat Abdalla, aliwataka wajasiriamali hao kutoridhika na masoko ya bidhaa zao kwenye maeneo husika na kubuni njia zingine mbadala.

Alisema kuna fursa nyingi za masoko kupitia bidhaa hizo hivyo ni vyema kuyatumia masoko hayo ili waweze kujiingizia kipato zaidi.

Kwa upande wao wajasiriamali hao walisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

“Tungekuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji tusingelalamika na ugumu wa maisha kwa sababu kilimo kina faida kubwa, lakini tatizo letu ni maji,” alisema Rehema Abasi kutoka Kijiji cha Bubwini.

Habari Kubwa