TARI yawapa mbinu wakulima wa zabibu

20Jan 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
TARI yawapa mbinu wakulima wa zabibu

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Makutupora, imewataka wakulima wa zabibu kuzingatia ushauri wa watafiti, ili kuongeza thamani ya zao hilo.

Mtafiti katika kitengo cha uchumi wa jamii wa kituo hicho, Devotha Mchau, alitoa rai hiyo jana alipozungumzia uongezaji thamani zao hilo katika ziara ya waandishi wa habari na watafiti waliotembelea kituo hicho.

Alisema zabibu hupandwa kwa misimu miwili, hivyo wakulima ni muhimu kuzingatia ushauri wa watafiti na kupata elimu ya utengenezaji mvinyo ili kujiongezea kipato.

"Unakuta wakulima wengi wanaendesha kilimo hicho bila kuwa na elimu ya kuongeza thamani zao hilo, ndiyo maana ninasisitiza wajitokeze katika vituo vya utafiti kupata mafunzo hayo," alisema Mchau.

Alisema wakulima wakipata elimu hiyo na kufuata taratibu za upandaji mpaka uvunaji, itasaidia kuvuna kwa wingi na kupata faida kubwa.

Mtafiti huyo aliwataka wakulima kufuata kanuni za utunzaji wa zao hilo ili kupata mavuno mengi.

"Zao la zabibu linahitaji sana uangalizi wakati wa kupanda mpaka mavuno, wakulima mkizingatia hayo, mtazidi kukua kiuchumi kupitia zao hilo," alisema Mchau.

Mtafiti mwingine wa kituo hicho, Stellah Hangambagi, alisema hali ya hewa ya Dodoma inaruhusu kulima zao hilo, hivyo wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo iwainue kiuchumi.

"Zao la zabibu linapendwa duniani kote na Dodoma imebarikiwa kuwa sehemu ambayo zao hilo linastawi, wakulima tumieni nafasi hii kujikwamua kiuchumi," alisema Hangambagi.

Alishukuru serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo imekuwa ikitoa  fedha kwa vituo vya utafiti wa kilimo....soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa