Ununuzi wa mazao watafutiwa mkakati

07Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ununuzi wa mazao watafutiwa mkakati

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, zimetakiwa kuandaa mikakati ya haraka kuainisha jinsi watakavyonunua mazao ya wakulima nchini.

mazao ya nafaka

Wakati NFRA imetakiwa kuainisha namna ya kununua nafaka za wakulima kwa upande wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, yenyewe imetakiwa kujikita katika ununuzi wa mazao mbalimbali ya wakulima ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko ya mazao ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, wakati akizungumza na wafanyakazi wa NFRA baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa.

Alisema kuwa wizara yake imekuwa ikihamasisha wakulima nchini kuzalisha kwa wingi mazao kwa ajili ya chakula na biashara, lakini inapofika hatua ya kuuza bei zinakuwa ndogo jambo ambalo serikali ya Rais John Pombe Magufuli haitalifumbia macho kamwe.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Hasunga, ameupongeza uongozi wa NFRA kwa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo nane ya kanda saba za wakala, ambapo ujenzi huo utaongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Mradi huo wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi umeanza kujengwa katika Manispaa ya Songea (Ruvuma), Dodoma, Mpanda (Katavi), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga Mjini (Shinyanga) na Babati (Manyara), ambapo serikali ya Tanzania na Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na Sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.

Hasunga alisema kuwa utakapokamilika ujenzi wa maghala na vihenge hivyo utapunguza gharama mbalimbali zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kununua dawa za kufukiza mahindi sambamba na gharama za kununua magunia ya kuhifadhia mahindi.

Katika hatua nyingine, waziri huyo amemtaka Kaimu Mtendaji Mkuu wa wakala NFRA, Vumilia Zikankuba, kuweka msisitizo zaidi wa kununua nafaka ya mahindi kwa kuwa katika kipindi chake serikali haitotoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mahindi badala yake NFRA ijipange kibiashara, ili kununua nafaka nyingi na kujiendesha.

Alisema huu sio muda wa NFRA kusubiri kupewa mtaji na serikali badala yake kufikiria tofauti na kuanza kufanya biashara ili kufikia walau ununuzi wa nafaka kwa tani zaidi ya 300,000.

Vilevile, ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kusimamia kwa weledi mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa, ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati kuwanufaisha wananchi.

    

 

Habari Kubwa