Vikundi kunufaika mikopo ya mil. 850/-

21May 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Vikundi kunufaika mikopo ya mil. 850/-

MFUKO wa uwezeshaji wananchi kiuchumi umejipanga kutoa mikopo 700 yenye thamani ya Sh. 850,000,000 kwa vikundi vya kiuchumi na wajasiriamali Unguja na Pemba ili kujikomboa na kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Hayo yalisemwa na Kaimu Waziri wa Uwezeshaji Wanawake na Watoto, Riziki Pembe Juma, wakati akiwasilisha makadirio ya  mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020-2021, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Unguja.

Pembe alisema miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kuchukuliwa na mfuko huo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa vikundi ambavyo vitapata mikopo hiyo ili miradi yao iwe endelevu na kuleta tija kwa walengwa.

Alisema ili kuhakikisha mikopo inayotolewa inatumika ipasavyo, watahakikisha wanafuatilia watu wote waliopewa mikopo hiyo pamoja na kuwapatia mafunzo.

“Wizara kwa mwaka wa fedha 2020-2021 imejipanga kuwawezesha wajasiriamali pamoja na vikundi vya Saccos na vyama vya ushirika ili wanachama wake waweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi,” alisema.

Alisema katika mwaka wa fedha 2020-2021, wamejipanga kuhakikisha vyama vya ushirika vinapiga hatua kubwa na tayari jumla ya vyama vya ushirika 186 vimesajiliwa kati ya hivyo 104, Pemba na 82 Unguja.

Kwa upande wa vyama vya ushirika alisema wananchi wamehamasika kujiunga huku wanawake wakionyesha mwamko mkubwa katika vikundi vya kuweka na kukopa.

Alisema kwa upande wa vyama vya ushirika wamejipanga kutoa elimu ya uendeshaji wake wenye tija pamoja na ukaguzi wa vitabu vya mahesabu na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Riziki aliliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya Sh. 18,510,451,000 kwa mwaka wa fedha 2020-2021, kati ya hizo Sh. 15,251,300,000 kwa matumizi ya kazi za kawaida na Sh. 10,095,200,000 kwa matumizi ya uendeshaji wa programu za wizara pamoja na matumizi ya mishahara.

Habari Kubwa