Wadau wa usafirishaji walilia ada ya leseni magari ya kukodi

20Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau wa usafirishaji walilia ada ya leseni magari ya kukodi

WAMILIKI na madereva wa magari maalum ya kukodi mkoani Arusha wameiomba Serikali kupitia upya ada ya leseni ya magari hayo ya shilingi milioni 1 iliyopendekezwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ili kuwezesha watoa huduma hao kuendelea kufanya biashara.

Wakizungumza katika kikao cha siku moja kilichofanyika mkoani humo cha kujadili ada hiyo, walisema wasafirishaji wengi hawakatai kutoa huduma, lakini ni vyema Serikali ikapunguza kiwango kwa kufanya utafiti wa kina sokoni.

“Kama watoa huduma tunapenda kuendelea kutoa huduma lakini ada iliyopendekezwa ni kubwa sana kulingana na aina ya biashara tunayofanya, na kupitia biashara hii tunaendesha maisha yetu, ikipita hii tunaweza kufunga biashara,” alisema Brian Fadhili.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji abiria (AKIBOA) mkoani Arusha, Locken Massawe, alisema wasafirishaji wanapaswa kujenga hoja ambazo zitaifanya Serikali kufanya uamuzi wa kupunguza au kubakiza ada hiyo.

 

“Hoja tutakazojenga ndio zitaamua kupunguza au kubakiza ada hiyo, maana Serikali hii ni sikivu na inafanya uamuzi kwa kuzingatia maoni ya, na ndio maana wako hapa japo wana uwezo wa kufanya uamuzi na ada hii ikabaki kama ilivyo,” alisema Massawe.

Massawe aliongeza kuwa Wizara izungumze na halmashauri nchini ili kutenga maeneo maalum ambayo magari haya yanaweza kupatikana ili kupunguza changamoto ya kutokuwa kwa watumiaji kujua sehemu za kupata huduma.

 

Kwa upande wake Meneja Leseni kutoka LATRA, Leo Ngowi, alisema lengo la mkutano huo ni kusikia maoni ya wadau na kuboresha utoaji wa huduma za usafirishaji nchini.

“Maoni  mtakayowasilisha katika mkutano huu tuangalie maeneo yote yanayohusisha makundi yote yaliyoainishwa, tusijikite tu kwenye maeneo machache maana yake maoni yenu yataboresha kanuni hizi na kuboresha mazingira ya usafirishaji,” alisema Ngowi.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uchukuzi, aliwahakikishia wadau hao kuwa maoni yao yatazingatiwa na kufanyiwa kazi kabla ya utekelezaji wake na kuwasisitiza wasafirishaji kutoa maoni kwa maandishi kupitia barua pepe ya Katibu Mkuu-Uchukuzi ili kuharakisha mchakato huo.

Habari Kubwa