Wajasiriamali Chunya wakopeshwa mil. 155/-

29Sep 2020
Grace Mwakalinga
Chunya
Nipashe
Wajasiriamali Chunya wakopeshwa mil. 155/-

JUMLA ya shilingi milioni 155 zimetolewa kwa vikundi 18 vya ujasiriamali vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya ikiwa ni lengo la serikali kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon, ndiye alikabidhi kiasi hicho cha fedha jana kwa vikundi 18 vya wajasiriamali ikiwa ni utekelezaji agizo la serikali kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mayeka alisema miongoni mwa wanufaika ni kundi la wanawake, vijana na wenye ulemavu, na kwamba moja ya masharti wanayotakiwa kuzingatia ni kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati ili na wengine waweze kukopeshwa.

Alisisitiza kuwa halmashauri haitasita kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa watakaokaidi kulipa mikopo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo, James Sunge, alisema kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, kiasi cha shilingi milioni 600 zimekopeshwa kwa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ambavyo tayari vilijisajili na kuwa na sifa ya kukopesheka na marejesho ya fedha hizo yanaenda vizuri.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Sophia Kumbuli, alisema utaratibu wa utoaji mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali ili kuwawezesha kufanya shughuli zao na kujikwamua na umaskini ni agizo la serikali, na kwamba wanaendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato kupitia mapato ya ndani ili kuwafikia watu wengi zaidi.

“Wanawake wengi sasa wanamiliki pesa na viwanda mbalimbali vya kuzalisha bidhaa, hali ambayo imesaidia kupunguza migogoro na vipigo ndani ya ndoa kwa sababu wanajitegemea," alisema Kumbuli.

Baadhi ya vikundi vilivyonufaika ni cha vijana Sabasaba ambapo Omary Mashauri ni miongoni mwa wanufaika, alisema kupitia mkopo wa shilingi milioni tano, uliwasaidia kufungua mradi wa kufungua mradi wa kiwanda cha kufyatua matofali.

Mwenyekiti wa kikundi cha kusindika mafuta ya alizeti, Ngailo Thobias, alisema walipewa mkopo wa Sh. milioni 14 ambazo walizitumia kuanzisha kiwanda na kutoa ajira, huku Evarist Fusi akisema kupitia mikopo hiyo wamesaidia kuongeza ajira kupitia uanzishwaji wa vikundi.

Wengine Beatrice Kalinga na Theresia Kayombo walisema wanawake wamenufaika na mikopo kwani hivi sasa wamefungua kiwanda cha kuchakata nafaka na kutengeneza batiki na wanasomesha watoto kupitia faida.

Habari Kubwa