Wakulima, wavuvi walia mazingira magumu

17Sep 2020
Rahma Suleiman
PEMBA
Nipashe
Wakulima, wavuvi walia mazingira magumu

WAVUVI na wakulima wa mwani wa Tumbe kisiwani Pemba, wamesema wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu ambayo baadhi yao husababisha kufariki dunia.

Waliyaeleza hayo juzi wakati walipotembelewa na mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefika kijiji hapo kwa ajili ya kuomba kura.

Masoud Abdallah Mwinyi ni miongoni mwa wavuvi wa kijiji hicho, alisema wavuvi wengi kijijini hapo wanapoteza maisha kwa sababu vyombo wanavyovulia ni vidogo.

“Tunakomba Maalim Seif ukiwa rais au kama una mpango wowote tufanyie ili tupate boti za kisasa za uvuvi na za uokozi ambazo zitatufaa sisi na wakulima wa mwani,” alisema Mwinyi kwa niaba ya wavuvi wenzake.

Naye mkulima wa mwani, zao ambalo hulimwa baharini, Halima Ali, alisema hata wao baadhi yao hufariki dunia baharini kutokana kina kikubwa cha maji na hawana zana za kisasa za kuendeleza kilimo hicho.

Alisema wamekuwa wakipoteza nguvu kazi kutokana na kulima mwani kwenye maji mengi kwa kutumia vyombo vidogo vya baharini ambavyo haviwezi kuhimili mawimbi makubwa ya bahari.

“Licha ya kwenda mbali na kina kikubwa cha maji, bei hii haituridhishi hata kidogo. Nyonga zote zimekufa kwa kuinama muda mrefu wakati bei ya mwani ni ndogo,” alisema mkulima huyo.

Kutokana na kilimo hicho, Maalim Seif alisema atakapoingia madarakani atahakikisha wavuvi wanakopeshwa boti za bei nafuu ili kuvua katika maji makubwa na kuwa salama.

Alisema atahakikish wavuvi wote wanakuwa na mawasiliano na wanamaji ili likitokea tatizo waweze kufanya mawasiliano ya haraka na kuokoa maisha yao.

“Tunakusudia kuyabadilisha maisha ya Wazanzibar kwa muda mfupi bila kuwabaguwa watu kwa sababu ya vyama vya siasa au dini,” alieleza Maalim Seif.

Akizungumzia zao la mwani, alisema katika serikali yake atahakikisha anaongeza bei ya mwani kutoka Sh. 600 hadi Sh. 1,000 kwa kilo na kuwapatia vifaa vyote ambavyo vitarahisisha katika kazi zao.

Mgombea huyo pia alisema endapo wananchi wa Zanzibar watamchagua, atahakikisha wakulima wa mwani wanapata faida kwa kuweka bei nzuri ambayo itakidhi machungu ya kilimo hicho.

Alieleza wanunuzi wa mwani wanawadhulumu wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei ya chini ya Sh. 600 kwa kilo moja.

Habari Kubwa