Watakaotafuna fedha za ushirika kukiona

18Jan 2020
Jaliwason Jasson
Babati
Nipashe
Watakaotafuna fedha za ushirika kukiona

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Manyara, imeapa kuwashughulikia watu wote watakaobainika kutafuna fedha za vyama vya ushirika.

Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Fidelis Kalungula, alisema juzi wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya utekelezaji kazi ya mkoa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba, mwaka jana.

"Tutaendelea kufuatilia vyama vya ushirika na waliohujumu tutahakikisha mali zilizohujumiwa zinarejeshwa na waliohujumu kufilisiwa," alisema Kalungula.

Aidha, alisema watachambua taarifa za ukaguzi wa hesabu ili kuona kila chama chenye udhaifu na kuufanyia kazi. Kalungula alisema watachambua kila chama ikiwamo kurejesha fedha na kuwafikisha mahakamani wahusika.

"Kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita Takukuru tulipokea malalamiko tisa juu ya vyama vya ushirika, hivyo inaonyesha katika vyama hivi kumekithiri ubadhirifu," alisema.

Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, walifanya uchunguzi na kuokoa Sh. milioni 13.4 na kati ya hizo Sh. milioni 5 ziliokolewa na kurejeshwa katika akaunti ya Chama Kikuu cha Ushirika (Rivacu).

Kwa mujibu wa Fidelis, katika kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa kwenye mstari miezi mitatu ijayo watayafanyia kazi malalamiko yote na kuwachukulia hatua wanaovihujumu vyama hivyo.

Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma, Sultan Ng'alanzi, aliwatahadharisha wenye tuhuma kwenye vyama hivyo kuwa makini na baadhi ya watu wanaowalaghai kuwapa msaada wa kumaliza kesi zao.

"Watu hao wanajiita maofisa wa Takukuru na kuwataka wakutane nao ili wawasaidie, msikubali kurubuniwa na muwaulize kama wana vitambulisho na mvione, lakini mkiwaona mje ofisi za Takukuru kutoa taarifa zao," alisema.

 

Habari Kubwa