Zanzibar yajikita uchumi wa uvuvi

29May 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Zanzibar yajikita uchumi wa uvuvi

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO) kwa kutumia meli yake aina ya Sehewa 11 iliyonunuliwa kutoka Srilanka imeanza shughuli za uvuvi katika eneo la ukanda wa bahari kuu.

Eneo la ukanda wa bahari kuu linaelezwa kuwa lina utajiri mkubwa wa samaki.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri, wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020-2021 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.

Mjawiri alisema uvuvi wa eneo la bahari kuu utaliwezesha shirika  kuuza samaki ndani ya nchi katika soko la utalii pamoja na kusafirisha nje ya nchi.

Alisema shirika hilo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha sekta ya uvuvi inaleta tija kwa taifa pamoja na kuwawezesha wananchi kuunda vikundi vya uvuvi.

Alieleza kuwapo kwa Shirika la Uvuvi kwa kiasi kikubwa kutaifanya sekta ya uvuvi kuongeza mchango wake kwa uchumi kwa taifa.

''Mheshimiwa napenda kumpongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa juhudi zake katika kulifufua ZAFICO ili lifanye kazi za uvuvi katika mwambao wa bahari kuu na kupunguza tatizo la uhaba wa samaki,'' alisema.

Aidha, alisema ZAFICO inatarajiwa kununua boti nyingine tano kwa ajili ya shughuli za uvuvi kwa vikundi mbalimbali vya vijana waliopo katika maeneo ya ukanda wa bahari kuu na kwa ajili ya doria.

Mjawiri alisema Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhakikisha uvuvi haramu unaotumia mitego iliyopigwa marufuku unadhibitiwa.

Alizitaja juhudi zilizochukuliwa katika kukabiliana na uvuvi haramu ni kufanya doria 172 katika maeneo yaliyotengwa ya hifadhi ya uvuvi wa mwambao Unguja na Pemba.

Alizitaja doria hizo ni ukanda wa hifadhi ya PECCA iliopo Pemba ambapo jumla ya doria 30 zilifanyika, huku ukanda wa hifadhi ya MIMCA iliopo Unguja jumla ya doria 41 zilifanyika.

Alieleza kuwa katika doria hizo jumla ya mitego ya samaki haramu 68 ilikamatwa na kuharibiwa ikiwamo nyavu zenye macho madogo ambazo hunasa samaki wa aina mbalimbali.

Alizipongeza kamati za uvuvi za halmashauri ya vijijini ambazo zimefanya kazi kubwa kupambana na uvuvi haramu, ikiwamo kusaidia kazi za doria.

Habari Kubwa