‘Amsha Ndoto’ kuhamasisha uwekaji akiba

28Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
‘Amsha Ndoto’ kuhamasisha uwekaji akiba

BENKI ya Azania (ABL), imezindua kampeni inayofahamika kama, ‘Amsha Ndoto’ yenye lengo la kuwahamasisha wateja wake na Watanzania kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kuweka akiba ili wawe na maisha imara kifedha baadaye.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania Charles Itembe Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa kampeni ya Amsha Ndoto 'Amsha Ndoto' .

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, kampeni hiyo itaendeshwa kwa miezi mitatu, kuanzia jana hadi Septemba 27, mwaka huu na itahusisha wateja wa zamani na wapya katika bidhaa mbili kuu za uwekaji akiba, ambazo ni: Ziada Akaunti(kwa ajili ya kila mmoja) na Watoto Akaunti (kwa ajili ya watoto tu).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa ABL, Charles Itembe, ili kustahili kupokea zawadi, wateja wanapaswa kuwa na akiba yenye thamani ya Sh. milioni moja kwenye akaunti zao na kuendelea ili kuwawezesha kustahili kuingia kwenye fainali ya droo na hatimaye kushinda.

Alisema washindi watatu watapatikana kila mwezi, kupitia kampeni hiyo na wateja wataweza kujishindia hadi mara mbili ya kiwango walichoweka kwenye akaunti na kiwango cha zawadi huweza kufikia Sh. milioni tatu.

Kuhusu vigezo vya washiriki, Itembe alisema kuwa wateja ni lazima waweke akiba ya Sh. 500,000 katika kipindi chote cha kampeni na mwaka mzima, na wale watakaoweka akiba kiasi cha Sh. milioni moja watapewa tokeni zitakazowawezesha kufuzu kwa ajili ya droo ya mwisho itakayowapata washindi.

“Tunawahamasisha Watanzania wote, wateja wetu wa sasa na wapya, wazazi na walezi kufungua akaunti hizi ili kuwa na uhakika wa maisha yao ya baadaye yaliyo salama. Kwa namna hii hawatahangaika kutafuta namna gani ya kuongeza mitaji, kulipia kodi za pango na kuwaandaa watoto wao kwa maisha ya baadaye,” alisema Itembe.

Promosheni hiyo yenye kaulimbiu inayosema, 'Weka akiba ushinde, tumwezeshe ada ya shule’, itawasilishwa kupitia radio na mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter, LinkedIn, Google Display placement na tovuti za ndani.