‘Biashara ya kuni, mkaa ni rasmi’

11Jun 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
‘Biashara ya kuni, mkaa ni rasmi’

BUNGE limeelezwa kuwa biashara ya kuni na mkaa ni rasmi na haina kizuizi chochote kwa mwananchi yeyote.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Zubeda Sakuru.

Katika swali lake, alihoji ongezeko la gharama za nishati nchini hasa umeme na gesi kusababisha kuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kuni na mkaa.

"Je, ni lini serikali itarasimisha biashara ya mkaa ili kupunguza makali ya maisha hasa kwa Watanzania wenye kipato duni," alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kanyasu, alisema biashara hiyo inafanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni za misitu pamoja na tangazo la serikali Na. 324 la 14/08/2016 na mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu wa mwaka 2007 uliofanyiwa marekebisho mwaka 2015.

"Hivyo, biashara hii ni rasmi na haina kizuizi chochote kwa mwananchi yeyote. Kinachotakiwa ni kufuata sheria na taratibu za kufanya biashara ambazo zimefafanuliwa vyema katika mwongozo wa uvunaji ambao unamtaka kila mvunaji wa miti kwa ajili ya nishati ya kuni na mkaa kuzifuata," alisema.

Alieleza kuwa kutokana na uhaba mkubwa wa nishati ya miti serikali inawahimiza Watanzania na wadau wote kuanzisha mashamba ya miti kwa ajili ya matumizi ya nishati.

Aliwaomba wabunge kuisaidia sekta ya misitu kwa kuishauri serikali kutoa ruzuku kwenye umeme, gesi na uzalishaji wa nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo inaongeza uharibifu wa misitu.

Hata hivyo, Kanyasu alifafanua kuwa kitu ambacho baadhi ya wafanyabiashara na wachoma mkaa hawatimizi ni pamoja na kutambua na kutenga maeneo ya misitu kwa ajili ya kutengeneza mkaa.

"Kila atakayehusika na shughuli ya biashara ya mkaa kutakiwa kusajiliwa na meneja wa misitu wa wilaya na atatakiwa kuwa na leseni, maombi ya usajili na leseni yanapaswa kupelekwa kwa ofisa misitu wa wilaya na kujadiliwa na kamati ya kusimamia uvunaji wa wilaya," alisema.

Pia alisema kila mfanyabiashara wa mkaa anatakiwa kulipia mrabaha kama ilivyoainishwa katika jedwali la 14 katika sheria ya misitu.

Habari Kubwa