‘Bila gesi, mafuta hakuna viwanda’

23Sep 2016
Peter Mkwavila
Nipashe
‘Bila gesi, mafuta hakuna viwanda’

PAMOJA na awamu ya tano kusisitiza kuwa serikali yake ni ya viwanda, imeelezwa kuwa bila kuwapo kwa gesi asilia na mafuta ya uhakika ni ndoto kufikia azma hiyo na na maendeleo kwa ujumla.

Ofisa Uhusiano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Francis Lupokela, alisema hayo jana alipokuwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mdeme, alipomkaribisha kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu shirika hilo.

Lupokela alisema lengo la TPDC kukutana na waandishi ni kuwajengea uwezo wa kulijua shirika hilo ili kutoa taarifa kwa jamii na serikali na kutumia rasilimali hizo kwa usahihi.

Alisema kama hakuna gesi asilia ya kutosha na mafuta ya uhakika, kamwe mpango wa Tanzania kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ni ndoto kufikiwa.

Pia alisema katika kuhakikisha shirika hilo linafanya kazi vizuri, ni lazima wananchi wajue wananufaikaje na rasilimali inayopatikana katika nchi yao.

Kwa upande wake, Mndeme aliwataka waandishi kutumia vyema talaamu yao kiuzalendo zaidi badala ya kuitangaza vibaya nchi yao.

"Ninyi katika taifa lolote hapa duniani ndio mnaotegemewa katika kuhabarisha umma mambo mbalimbali yanayotokea. Ninawaomba tangazeni vyema nchi yetu ya Tanzania pamoja na maliasili zilizopo ili kuwafanya wageni kuvutiwa na kuwafanya washawishike kuwekeza.

"Tunaelekea katika nchi ya uchumi wa kati wa viwanda, hivyo tunahitaji kuwa na gesi ya kutosha, umeme na mafuta. Wanahabari mkitumia vyema kalamu zenu kwa uzalendo tutapata wawekezaji kwa ajili ya kujenga viwanda au kuchimba gesi ya kutosha na hiyo itachangia maendeleo ya nchi.

"Iwapo Tanzania itatangazwa kiuzalendo, itasababisha watu wengi kuvutiwa na kuwekeza katika nchi na itasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini," alisema Mndeme.

Habari Kubwa