‘Marufuku uokotaji karafuu zinazoanguka’

15Sep 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
‘Marufuku uokotaji karafuu zinazoanguka’

WIZARA ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imepiga marufuku uokotaji wa karafuu zinazoanguka chini maarufu kwa jina la 'mpeta' baada ya kubainika kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kusababisha pia wanafunzi kutoroka shule.

Hayo yalisemwa jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi na Waziri wa wizara hiyo, Omar Said Shaaban, wakati akitoa ufafanuzi na kujibu swali la Mwakilishi wa Viti Maalum Kaskazini Pemba, Shadya Suleiman, aliyetaka kujua sababu za serikali kupiga marufuku uokotaji wa karafuu zinazoanguka chini.

Alisema kumejitokeza matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika kipindi cha msimu wa mavuno ya karafuu na kundi hilo hujishughulisha uokotaji wa zinazoanguka chini.

Kadhalika alisema utafiti unaonyesha kwamba matukio hayo huongezeka katika msimu wa mavuno na wanawake na watoto ndiyo wengi wanaojitokeza katika kazi za kuokota karafuu hizo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imepiga marufuku uokotaji wa karafuu zinazoanguka chini kwa sababu tumefanya utafiti na kubaini kuwapo kwa kasi ya matukio ya udhalilishaji wa kijinsia na watoto kutoroka shule,” alisema.

Aidha aliwataka wakulima wa karafuu kuongeza bidii kuhakikisha kwamba wanapata karafuu daraja la kwanza ili kupata kipato kikubwa.

Alisema kazi ya kupata karafuu daraja la kwanza masharti yake wakulima wengi wa karafuu wanayafahamu ikiwamo kuanika vizuri karafuu hizo na kukauka.

“Tunawaomba wakulima wetu kuhakikisha wanapata daraja la kwanza la karafuu ambapo masharti yake kukauka vizuri na kuzisafisha taka zote,” alisema.