‘Serikali haijazuia utafiti mbegu GMO’

02Jul 2019
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
‘Serikali haijazuia utafiti mbegu GMO’

SERIKALI imesema utafiti kuhusu mbegu za Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO), haujawahi kuzuiwa wala kuchoma moto majaribio yake yanayofanyika hapa nchini bali unaendelea kufanyika kwa baraka zote za serikali na utakapokamilika maamuzi yatatolewa.

Majaribio ya utafiti wa mbegu za GMO yanafanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Makutupora kilichopo mkoani Dodoma, kuhusu mbegu za mahindi na Taasisi ya Utafiti Mikocheni iliyopo jijini Dar es Salaam, kuhusu mbegu za mihogo.

Kauli ya serikali ya kuendelea na utafiti wa mbegu za GMO imekuja ikiwa takribani miezi minne iliyopita kufuatia Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigimwa, kueleza uamuzi wa serikali kusitisha utafiti huo unaofanyika katika taasisi hizo mbili za utafiti.

Akizungumza katika mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO kwa Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mratibu wa Utafiti wa Bioteknolojia za kilimo Tanzania kutoka Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Fred Tairo, alisema kwa sasa utafiti huo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali katika vituo hivyo.

Alisema TARI haijaacha kufanya utafiti wa GMO tangu ilivyoanza na unaendelea na umeonyesha matokeo chanya kwa mbegu zote mbili.

Dk. Tairo, alisema watu pamoja na vyombo vya habari nchini walielewa vibaya kuhusu taarifa zilizotolewa na kwamba serikali ilitaka watafiti wafuate utaratibu wa kutoa matokeo waliyokuwa wanayapata kwenye majaribio hayo ili kuondoa mkanganyiko.

Mtafiti huyo alisema msimamo wa serikali ni kuendelea na utafiti wa GMO ili uweze kukamilika katika hatua zake muhimu na kisha utakapokamilika utapeleka katika mamlaka husika kwa ajili ya kutoa maamuzi.

Habari Kubwa