‘Vipanya’ vyapigwa marufuku Dodoma

21Mar 2017
Peter Mkwavila
Nipashe
‘Vipanya’ vyapigwa marufuku Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoa wa Dodoma, umepiga marufuku usafiri wa daladala wa mabasi madogo maarufu ‘vipanya’ kufanya safari katikati ya mji.

Aidha, imesitisha utoaji wa leseni mpya kwa ajili ya mabasi hayo madogo (Hiace), badala yake itaanza kutoa kwa magari makubwa aina ya Tata na Eicher, kwa ajili ya usafiri wa katikati ya mji.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Mkoa wa Dodoma, Conrad Shio, akizungumza katika kikao cha Baraza la Biashara la wilaya kilichofanyika juzi, alisema waliamua kufanya hivyo kutokana na kupewa agizo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema agizo hilo liliwataka kuanzia sasa kuacha kutoa leseni kwa daladala zinazofanya biashara katikati ya mji badala yake watoe kwa magari makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi kwa wakati mmoja.

"Daladala ndogo kwa sasa hivi hazitapewa leseni za kuhudumia katika ya mjini, hili ni agizo kutoka kwa Waziri Mkuu na kutaka kutoa mabasi makubwa kama Tata na Eicher,’’ alisema.

Alisema daladala hizo zilizokuwa zikifanya safari zake katikati ya mji zitaanza kwenda nje ya mji ili kupunguza msongamano.

Alisema kuanzia jana (Jumatatu), wataanza kutoa leseni kwa kampuni tu na si kwa mtu mmoja mmoja lengo likiwa ni kuondoa msongamano wa magari katika ya mji na makao makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dodoma (Uwedo), Jackson Bandyaji, akizungumza kwa niaba ya wenye daladala alisema maagizo hayo waliyapokea na kuanza kuyafanyia kazi.

“Hivi sasa Dodoma ni makao makuu ya nchi, lazima tukiri na kukubaliana na changamoto mbalimbali na tutatakiwa kukaa kwa pamoja na Sumatra ili tuweze kuzijadili,” alisema Bandyaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, aliwataka wafanyabiashara hao kutumia ujio wa makao makuu ya nchi kujiongezea kipato kwa kufanya biashara zao ziwe na ubora.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho cha baraza, aliwataka wafanyabiashara mjini humo kuhakikisha biashara zote muhimu
zinapatikana.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu ‘wamachinga’ kuacha kupanga biadhaa pembezoni mwa barabara kutokana wanahatarisha maisha yao.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godfrey Kunambi, alisema kumekuwa na changamoto ya utendaji kazi kati ya Manispaa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA).

Alisema wakati CDA inaanzishwa 1974, kulikuwa na kata 21, lakini sasa zipo 41 na changamoto za ununuaji wa viwanja ndani ya kata za zamani, unauziwa na serikali ya kijiji na kuhitaji maboresho ya sheria.

Habari Kubwa