‘Wafanyabiashara wakwepa kodi kiama chaja’

09Feb 2016
Daniel Mkate
Mwanza
Nipashe
‘Wafanyabiashara wakwepa kodi kiama chaja’

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, amesema wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi nchini, wajiandae kufungiwa biashara zao kutokana na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacius Likwelile

Akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara na maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) jijini Mwanza mwishoni mwa wiki,

Dk. Likwalile alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya biashara na kukwepa kulipa kodi ambayo inasaidia maendeleo ya nchi. “Hivi sasa kila sehemu tumeweka watu wetu ili kuwafuatilia wale wasiolipa kodi…hivyo mfanyabiashara asiyelipa kodi ajiandae kufungiwa biashara yake,” alisema Dk. Likwelile.

Aidha, Dk. Likwalile aliwataka wafanyabiashara kushirikiana na maafisa wa TRA katika kukusanya mapato ili kuiletea maendeleo nchi. Alisema sifa ya mfanyabiashara mzuri ni kuhakikisha analipa kodi badala ya kukwepa, pia kuonyesha uzalendo ili kuiletea nchi maendeleo kwa kasi.

“Tuwe na uchungu na nchi yetu, tuhakikisha kila mtu analipa kodi…zipo hoteli kubwa na nzuri, lakini hazitoi malipo ya stakabadhi hivyo kuibia nchi mapato,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa stakabadhi pale wanapofanya biashara zao na wala wasidhani kutoa stakabadhi hizo ni kufanya hisani kwa mteja.

Dk. Likwelile alisema mapato yanayokusanywa na TRA yanasaidia kulipa mishahara kwa wafanyakazi wa serikali zaidi ya Sh. bilioni 535 kwa mwezi mmoja.
Naye mfanyabiashara Abubakar Hassan, aliishauri TRA kuachana na vitisho wakati wa ukusanyaji wa kodi ambayo ni haki ya kila mfanyabiashara kufanya hivyo.

Aidha, alisema mamlaka hiyo iachane na tabia ya kuwahofia wafanyabiashara ‘majambazi’ ambao wamekuwa hawafuatiliwi kudaiwa kodi ya serikali. Tausi Hariri, mfanyabiashara wa jijini humo, alisema ukusanyaji wa mapato lazima uwe na mahusiano mazuri na wafanyabiashara wote ili kuiletea maendeleo nchi.