53 walivyonusurika kuzama baharini

06Apr 2017
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
53 walivyonusurika kuzama baharini

WAVUVI 53 wamenusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wakiitumia kwa shughuli za uvuvi baharini katika kisiwa cha Tumbatu kuzama.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Hassan Ali Kombo, alisema wavuvi waliondokea Mtoni Mjini Unguja na kupata ajali hiyo juzi saa 4:00 asubuhi wakiwa katika shughuli zao za uvuvi.

Hassan alisema chanzo cha ajali hiyo ni mawimbi makali baharini na upepo uliokuwa ukivuma na kusababisha boti hiyo kuzama.

Alisema wavuvi hao walijiokoa kwa kuogolea ili kunusuru maisha yao.

Hassan alifafanua kuwa wavuvi 42 waliokolewa katika kisiwa cha Tumbatu juzi saa 4:00 usiku.

Aidha, alisema kati ya wavuvi hao 53, mmoja Khatib Khamis, aliokolewa na meli ya Azam Silink namba mbili akiwa anaelea baharini iliyokuwa ikitokea kisiwani Pemba kuelekea Unguja.

Alisema wavuvi wengine 10 kati ya hao waliokolewa jana katika bahari ya Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini `B' na wapo katika Hospitali ya Kivunge kwa matibabu.

“Wavuvi waliokolewa juzi wamesharejea katika makazi yao isipokuwa 10 waliokolewa jana, wapo Hospitali ya Kivunge kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri," alifafanua Hassan.

Aidha, aliwataka wavuvi kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika na kuhakikisha wanakuwa na mawasiliano kila wakati wanapokuwa baharini ili wakipatwa matatizo, taarifa zao zinafahamike haraka.

Mratibu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wavuvi wa Kojani, Omar Mohammed Ali, alisema wavuvi 53 walionusurika kufa ni wanachama wao katika jumuiya hiyo.

Omar alisema baada ya boti ya uvuvi iitwayo `Shoo' waliyokuwa wamepanda kwa shughuli za uvuvi kuzama, wavuvi hao waliogolea hadi katika maeneo ya nchi kavu na kuomba msaada.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdallah Kombo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Abdallah alisema mamlaka yake kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Vikosi vya Uokoaji na Kuzuia Magendo Baharini (KMKM), viliwasaidia wavuvi hao.

Habari Kubwa