90% ya Watanzania wanatumia mkaa, kuni

02Sep 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
90% ya Watanzania wanatumia mkaa, kuni

WAKATI serikali ikisisitiza kutumika kwa nishati ya gesi badala ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani, imebainika kuwa zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania hususani wanaoishi mijini wanatumia nishati ya mkaa.

Hiyo inatokana na Watanzania kushindwa kumudu gharama za kununua gesi na hivyo kulazimika kutumia nishati ya mkaa na kuni.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la kuhifadhi misitu Tanzania (TFCG), Charles Meshack, alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa Tanzania, uliowashirikisha watendaji na wadau wa misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani hapa.

Alisema pamoja na kuwapo kwa matumizi makubwa ya mkaa, hakuna sera inayosimamia nishati hiyo hali inayosababisha halmashauri nyingi kupoteza mapato yanayotokana na mkaa.

Kufuatia hali hiyo TFCG kwa kushirikiana na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la kuendeleza nishati asilia Tanzania (TaTEDO), chini ya ufadhili wa Shirika la maendeleo na ushirikiano la Uswisi, wameanzisha mradi wa majaribio wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa na sasa mradi huo unatekelezwa katika Wilaya ya Mvomero.

Kwa upande wake Meneja mradi wa TFCG, Charles Leonard, alisema mradi huo wa miaka minne ulianza Desemba 2015 hadi 2019 na mojawapo ya unalengo ni kuanzisha mfumo wa usimamizi endelevu wa mnyororo wa thamani wa mkaa na mazao mengine ya misitu katika vijiji 30, wilayani Kilosa, Mvomero na Morogoro.

Alisema mradi pia unatoa mafunzo kwa halmashauri za vijiji na kamati za maliasili na misitu za vijiji na wachoma mkaa namna ya kutunza, kuvuna misitu na kuchoma mkaa pia wachoma mkaa wanajengewa uwezo wa kujisajili ili waweze kutambulika.

Awali, akizindua mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly, aliwataka maofisa misitu kuacha kutoa vibali vya mkaa bila ya kujua mahali unakotoka, ili kuepuka ukataji miti ovyo wilayani humo.

Aidha, alipiga marufuku uvunaji wa miti aina ya mipingo wilayani humo, inayochomwa mkaa na kuuzwa kuni huku akiitaka Idara ya misitu kufuatilia na kusimamia miti hiyo ili isiendelee kuvunwa.

Habari Kubwa