Aahidi ubalozi kutangaza Mlima Kilimanjaro

05Dec 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Aahidi ubalozi kutangaza Mlima Kilimanjaro

MWANAMKE pekee maarufu aliyevunja rekodi ya dunia ya Kitabu cha Guinness kwa kushiriki na kushinda mara 17 mbio za kimataifa kati ya mwaka 2012/2013, Parvaneh Moayed, ameahidi kuwa balozi wa kimataifa wa kutangaza vivutio vya utalii wa Mlima Kilimanjaro.

Parvaneh ambaye ni raia wa Iran na Marekani, anayeshikilia rekodi ya Guinness ya San Antonio na Bad Water Ultra Marathon, alitoa ahadi hiyo jana wakati Kampuni ya Kilismile Trails Ltd., ilipotangaza nia yake ya kubeba jukumu la kulipigia debe lango la Umbwe la kuingia na kupanda Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.

“Mimi na wenzangu 17 kutoka mataifa mbalimbali tutakimbia ndani ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na nia yetu hasa ni kusaidia kuutangaza mlima huu duniani. Si kazi rahisi, lakini tunataka kuweka rekodi nyingine ya ukimbiaji wa tofauti ambao haujawahi kufanyika katika kuutangaza Mlima Kilimanjaro,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kilismile Trails Ltd, Hamadi Gao, alisema upandaji wa Mlima Kilimanjaro uko tofauti na wageni wengine wanavyopanda, kwa kuwa utahusu ukimbiaji baada ya kufika kilele cha uhuru.

“Wapandaji hawa wanaokimbia watapita kilele cha Uhuru, Kibo Heart, Mawenzi Heart, Horombo na watamalizia Marangu Gate (lango). Hizi mbio watu wanafanya, lakini sisi tumeamua kufanya kwa mapana zaidi kupitia Kilimanjaro Extrem Marathon…tumefanya survey (utafiti) zaidi ya mara nne, tutapanda Desemba 4 na kuanza kukimbia Desemba 9, mwaka huu,” alisema.

Gao alisema wameamua kulitumia lango la Umbwe lililopo Kibosho, Wilaya ya Moshi kuutangaza Mlima Kilimanjaro na vivutio vyake, kwa sababu wageni wengi hawaitumii njia hiyo kupanda Mlima Kilimanjaro, na ndio maana wameamua kuja na ubunifu huo.

Kwa upande wake, Michael Gawron, Mkurugenzi mwenza wa kampeni hiyo, alisema upandaji wa mlima kwa aina ya kukimbia, utakuwa ukifanyika kila mwaka na kwa mwaka huu utahusisha wakimbiaji 17.

Kwa kawaida, safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro humpitisha mpandaji katika kanda za hali ya hewa tofauti kuanzia ile ya nchi za tropiki hadi arktiki. Kilele cha Kibo chenye urefu wa mita 5,895, ndicho kivutio kikubwa kwa wageni kutokana na kufunikwa na theruji.

Katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, kuna njia sita za kupanda hadi kileleni na njia iliyo rahisi na iliyo maarufu zaidi ni ile ya kuanzia lango la Marangu ambako ndiyo makao makuu ya hifadhi.

 

Habari Kubwa