Abiria wachakachua tiketi kivuko Kigamboni

07Feb 2016
Moshi Lusonzo
Nipashe Jumapili
Abiria wachakachua tiketi kivuko Kigamboni

MBINU mpya ya wizi wa mapato inatumika katika kivuko cha Kigambo jijini Dar es Salaam na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu kwa kuchakachua tiketi.

Katika uchunguzi uliofanywa na Nipashe, imebaini wizi huo unafanyika na watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) kwa kuacha kwa makusudi kuzitambua baadhi ya tiketi za elekroniki na kuonekana hazijatumika.
Wizi huo unaikosesha serikali mamilioni ya pesa kila siku, unafanyika na watu wanaokata tiketi na ukaguzi katika vituo vya Magogoni na Kigamboni.
Mwaka 2013, Rais Dk. John Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi, alitoa muda wa siku 60 kwa Temesa kuhakikisha wanaweka mashine ya umeme itakayoweza kutoa tiketi za abiria na mizigo ili kuzuia wizi.
Kauli hiiyo ilirudiwa tena na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh.Prof. Makame Mbarawa, aliagiza kufungwa haraka mfumo kamili wa elekroniki katika kivuko hicho ili kudhibiti mapato yanayopotea kiholela.
Imeripotiwa asilimia 20 kati ya abiria 60,000 wanaotumia kivuko cha Mv Magogoni na Mv Kigamboni kila siku wanaonekana wakivuka bila kulipa nauli.

WIZI UNAOFANYIKA
Katika uchunguzi huo, imeonekana kuna mtandao mkubwa wa watumishi ndani ya Wizara hiyo na Tamesa, wananufaika na ufisadi huo, kiasi ambacho inakuwa vigumu kutekeleza maagizo ya viongozi wao.
Wanajua kufungwa kwa mtambo huo, hakutakuwa na nafasi ya kuzoa mamlioni ya pesa kama ilivyo sasa.
Taarifa za kuaminika zinasema wizi huo unaofanyika umewatajirisha wengi na mtu akipangiwa kufanya kazi katika vituo hivyo anatajirika haraka.
Kwa kawaida abiria anapofika katika kituo kimojawapo anakata tiketi zenye alama maalum (Barcon), kisha anakwenda kwa mtu mwingine ambaye kazi yake ni kuzitambua kwa kutumia mashine maalum.
Mashine hizo zinazotumia mionzi, inapomulika alama hizo. inatambua tiketi na kuziingiza katika orodha kamili kwenye kompyuta.
Hata hivyo, watumishi hao walionekana kukwepa kuzitambua, badala yake idadi kubwa ya tiketi zilionekana zikikusanywa bila kumulikwa na mashine hizo.
Kwa kitendo hicho tiketi hizo zinaonekana bado hazijatumika, hivyo pesa zake zinaishia mifukoni mwa watu hao.

WANANCHI WAKIRI
Baadhi ya wananchi wanaotumia vivuko hivyo wamekiri tiketi zao kutopitia katika mashine hizo, badala yake wafanyakazi hao mara wanapochukua kutoka kwa abiria wanaitupa katika pipa la takataka.
Mohamed Hamdan mkazi wa Kigamboni, alisema yeye kila siku anatumia vivuko hivyo, lakini mara chache tiketi zake zinathibitishwa na mashine hizo.
“Suala la wafanyakazi wa kivuko kutozimulika tiketi ni jambo la kawaida, utakuta anakusanya tiketi nyingi lakini zinazomulikwa ni chache sana,” alisema Hamdan.
Salima Saidi, mkazi wa Vijibweni aliomba serikali kufanya uchunguzi maalum kujua kiasi gani cha pesa kilichopotea kutokana na uzembe huo unaofanywa na wafanyakazi waliaminiwa na umma.
“Serikali inatakiwa kufuatilia suala hili, hatuwezi kusema mashine zile zilizonunuliwa na serikali hazina maana, lazima hawa watu wanakwepa kuzitambua tiketi kwa nia mbaya,” aliongeza kusema.

MBARAWA ASHTUKA
Katika ziara yake aliyoifanya januari 12 mwaka huu, Waziri Profesa Mbarawa, aliona dalili ya kuwapo kwa harufu ya ufisadi na kuamuru ndani miezi mitatu wawe wamefunga mfumo kamili wa elekroniki.
“Nawapa miezi mitatu muwe mmefunga mfumo kamili wa kupokea nauli wa elektroniki ambao utadhibiti ukwepaji wa kulipa nauli ili kuongeza mapato na kufikia shilingi milioni 25 kwa siku,” alisisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa kufunga mfumo huo tiketi zitambuliwa haraka mara abiria anapokata, hivyo kuondoa mwanya wa watu kuchakachua.

NI KOSA-TAMESA
Akizungumzia suala hilo, kaimu Afisa mtendaji wa Tamesa, Mhandisi manase Le-Kujan, alisema ni kosa kwa wafanyakazi wa vivuko hivyo kuacha kuzitambua tiketi kwa mashine hizo.
Alisema mashine hizo zina kazi ya kuhakiki tiketi na zinapoitambua inakuwa mwisho wa kufanya kazi, hivyo haziwezi kutumiwa na watu wengine.
‘Kuziacha bila kuzitambua na mashine ni rahisi watu wengine kuzitumia mara ya pili, kama wanafanya hivyo hilo ni kosa,” alisema Le-Kujan.
Hata hivyo alisemakitendo cha kuacha kuzitambua tiketi hizo si kwamba mapato yanapotea, bali idadi ya mapato yanabaki kuwa yaleyale.

Habari Kubwa