Adha kufuata huduma afya kuwa historia

27Jan 2019
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe Jumapili
Adha kufuata huduma afya kuwa historia

WAKAZI wa wilaya ya Bukoba, huenda wakaondokana na adha waliokuwa wakipambana nayo ya kusongamana katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera kwa ajili ya huduma za matibabu baada ya kuanza kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya.

HOSPITALI YA RUFABNI MKOA WA KAGERA

Wananchi hao hasa kutoka tarafa za Bugabo na Kyamtwara, wamekuwa wakishindwa kuitumia hospitali teule ya wilaya, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ), Dayosisi ya Kaskazini Magharibi  kutokana na jiografia mbaya ya halmashauri hiyo.

 

Miongoni mwa wananchi waliozungumzia ujenzi wa hospitali hiyo katika eneo la Katerero, ni Laurent Erasto, ambaye alidai kuwa tangu nchi ipate uhuru, hawakuwahi kuwa na hospitali ya wilaya ya serikali na kuwa ujenzi wake utakuwa  mkombozi kwao.

 

Naye Hajati Seif, mkazi wa Katerero, alisema kwa miaka mingi wamekuwa wakihangaika kufuata huduma mbali na kuwa hospitali hiyo itawapunguzia usumbufu na gharama hasa kinamama na watoto.

 

“Wanawake na watoto tumepata shida sana, hospitali teule ilipo hapaendeki ni mbali pia. Miaka yote kama tatizo ulilonalo limeshindwa kutatulika katika zahanati yetu, tumekuwa tukilazimika kwenda hospitali ya rufani Bukoba mjini au Kagondo wilayani Muleba,” alisema.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa hospitali hiyo uliokwenda sambamba na wananchi kujitolea nguvu zao kushiriki kuchimba msingi, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo, alisema ujenzi huo kwa hatua za awali utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.8.

 

Kinawiro aliwaomba wananchi kuendelea kujitolea katika ujenzi wa hospitali hiyo kwa sababu huduma ni kwa ajili yao na kumshukuru Rais John Magufuli kwa jitihada zake za kuboresha huduma za afya nchini.

 

“Msikae mkasubiri eti serikali itajenga, mwendelee kujitolea nguvu zenu kila inapowezekana. Lengo letu ni moja tu la kukamilisha hospitali hii mapema iwezekanavyo ili ianze kutoa huduma,” alisema.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Murshid Ngeze, alisema wananchi hasa kutoka tarafa za Kyamtwala na Bugabo, wanapata shida ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya na kumshukuru Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza, kwa jitihada zake za kuwezesha ujenzi huo kuanza.

 

“Kuna umuhimu mkubwa wa kupata hospitali yetu ili kuwapunguzia wananchi usumbufu hasa wanaotoka katika tarafa za Kyamtwara na Bugabo lakini pia kupata huduma za afya zilizo bora. Hospitali inayotumika kama hospitali teule ya wilaya, itaendelea kuwahudumia wananchi walioko tarafa ya Rubale maana ndio walioko karibu” alisema.

 

 

Habari Kubwa