AfDB yaahidi kusaidia kilimo, viwanda EAC

23Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
AfDB yaahidi kusaidia kilimo, viwanda EAC

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeahidi kutoa msaada zaidi katika sekta ya kilimo na viwanda katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC).

Ahadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa ukanda wa Afrika Mashariki wa benki hiyo, Gabriel Negatu, wakati alipokwenda kujitambulisha ofisini kwa Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko juzi.

Alisema uwekezaji katika kilimo na viwanda ni jambo linalopewa umuhimu kwa maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuonana na Katibu Mkuu, Negatu alisema ni wazi kwamba uchumi wa nchi za Afrika Mashariki umejikita zaidi katika kilimo ambacho ni mhimili wa uchumi unaochangia asilimia 75 hadi 90 ya idadi ya watu wake.

Alisema ili kukidhi masoko ya kikanda na kimataifa, bidhaa za mazao zinatoa fursa kwa ukuaji wa viwanda.

“Mafanikio katika kilimo ni muhimu kwa ajili ya kuwainua wananchi kutoka hali ya umaskini kwa sababu inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya idadi ya watu katika nchi wanachama ambao wengi wao wanaishi katika maeneo ya vijijini,” alisema.

Aidha, alisema sekta ya kilimo inaboresha maisha ya watu wa vijijini na mijini.

Kwa upande wake, Balozi Mfumukeko, aliishukuru AfDB kwa kuchangia matangamano wa Afrika Mashariki ana anaahidi kwamba jumuiya hiyo itaimarisha ushirikiano na kukua zaidi.

Alisema kwa miaka mitano iliyopita, AfDB, imetoa misaada katika miradi mbalimbali akitaja kwa mfano upembuzi yakinifu na ujenzi wa miundombinu ya barabara kutoka Nyakanazi –Kasulu, Rumonge Bujumbura na Lusahunga –Rusumo, Kayonza, Masaka-Mutukula-Kyaka-Bugen.

Habari Kubwa