AfDB yaombwa kuendelea kufadhili miradi barabara

20Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
AfDB yaombwa kuendelea kufadhili miradi barabara

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuendelea kutekeleza mkakati wake wa ufadhili wa miradi mbalimbali nchini ikiwamo ya barabara.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, picha mtandao

Aliyasema hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo kuhusiana na maendeleo na utekelezaji wa miradi ya barabara inayofadhiliwa na benki hiyo.

“Tunawashukuru AfDB kwa kuwa miongoni mwa wadau muhimu katika kutoa ufadhili wa utekelezaji na uboreshaji wa barabara nyingi nchini, tunaomba muendelee na ufadhili kwani bado tunahitaji kuendelea kuunganisha mtandao wa barabara kati yetu na nchi jirani,” alisema Waziri Kamwelwe.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha miaka 11 iliyopita Benki hiyo imetoa zaidi ya Sh. Trilioni mbili kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 1,655 ambapo kati ya hizo kilometa 1,168 zimeshakamilika na 487 zinaendelea kujengwa.

Alitaja baadhi ya miradi ya barabara iliyofadhiliwa na Benki hiyo na ambayo imekamilika kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ni ukarabati wa barabara ya Arusha - Namanga (km 105), barabara ya Singida - Babati - Minjingu ( km 223.5), barabara ya Iringa - Dodoma (km 260) na barabara ya Namtumbo - Tunduru (km 193).

Ameongeza kuwa miradi mingine ya barabara inayoendelea kutekelezwa kupitia ufadhili wa Benki hiyo ni ujenzi wa barabara ya Tabora-Koga- Mpanda (km 349), barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka kwa Awamu ya II, barabara ya Tanga – Pangani - Bagamoyo (km 246), barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma, na ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato jijini humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB, Amos Cheptoo, alisema benki yake itaendelea kuunga mkono na kufadhili miradi mbalimbali ikiwamo ya barabara lengo ni kuifanya Afrika kuendelea kiuchumi.

Alisema lengo la kuja kwake Tanzania ni kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo ili kuona maendeleo yake.

Habari Kubwa