Ahimiza uwekezaji zaidi bima majanga ya moto

20Jul 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Ahimiza uwekezaji zaidi bima majanga ya moto

SERIKALI imewaomba wadau wa bima kuwekeza zaidi katika huduma ya utoaji kinga za majanga ya moto ili kuwavutia wawekezaji kuwa na uhakika wa biashara wanazowekeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, wakati wa maazimisho ya Siku ya Bima ya Kanda ya Kati.

Dk. Mahenge alisema kuna kila sababu ya kampuni hizo kutoa huduma ya kinga ya majanga ya moto, afya na nyingine ambazo ni muhimu kwa jamii ili kuwavutia wawekezaji kutokana na kwamba watakuwa na uhakika na biashara wanazofanya.

Alisema kwa sasa taifa linaelekea katika uchumi wa viwanda na kila mmoja anapaswa kuangalia fursa inayoweza kumpa faida yeye binafsi na taifa kwa ujumla na kuifanyia kazi kiufanisi.

“Naomba kampuni za bima changamkieni fursa za uwekezaji katika huduma ya kinga, lengo ni kuona kila mmoja anatoa huduma za uhakika,” Dk. Mahenge alishauri.

Alisema bima ni muhimu kwa sababu ni mpango ambao unaisadia jamii kuepuka kuanguka kiuchumi kutokana na kwamba watakuwa na uhakika wa usalama wao.

Kiongozi huyo wa mkoa pia alisema hakuna sababu ya kubagua watu katika utoaji wa huduma za afya kwa kampuni za bima.