Airtel fursa yaendelea kubadilisha maisha ya wajasiriamali vijana

09Feb 2016
WAANDISHI WETU
Dar
Nipashe
Airtel fursa yaendelea kubadilisha maisha ya wajasiriamali vijana

WAFANYAKAZI wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel wameungana na mpango Airtel Fursa kuwafikia vijana wajasiriamali, kwa kusaidia kukarabati bucha la kijana mmoja mkoani Morogoro.

Mwishoni mwa wiki, wafanyakazi hao walimsaidia kijana Hashim Mikidadi, anayejihusisha na kuuza bucha la nyama kwa kukarabati duka lake lililopo stendi ya mabasi Ngerengere, mjini Morogoro. Akizungumza wakati wa ukarabati wa bucha hilo, Ofisa mauzo wa Airtel, Aminata Keita, alisema: “Airtel tunajali sana jamii yetu inayotuzunguka hivyo tunaelewa changamoto nyingi ambazo vijana wamekuwa wakikutana nazo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, ukosefu wa mtaji wa kuanzisha biashara zao na mambo mengine mengi.” “Msaada wetu kama wafanyakazi wa Airtel ni kuunga mkono mpango wa kampuni yetu ya kusaidia vijana hapa nchini ujulikanao kama Airtel Fursa katika kusaidia vijana wetu kwa kuwaonyesha njia ili waweze kuinua jamii inayowazunguka na kufikia ndoto zao,” alisema. Aliongeza kuwa: “Airtel Fursa itamwekea vifaa vya kisasa vikiwamo vifaa vya kukatia nyama, jokofu la kisasa la kuhifadhia nyama na vifaa vingine vinavyohitajika kwa kazi za bucha. Vifaa hivyo na gharama za utengenezaji vimegharimu kiasi cha Sh. milioni tisa.” Kwa upande wake, Hashim aliishukuru Airtel kwa kumpatia fursa kwani ni vijana wengi wanaohitaji msaada. “Nilianza nikiwa sina kitu. Lakini leo Airtel imeinua maisha yangu na kuniwezesha kuwapatia ajira vijana wenzangu waliokuwa mtaani bila kazi.” Airtel Fursa awamu ya kwanza ulianza Mei mwaka jana na hadi sasa umekwishawafikia zaidi ya vijana 3,000 kwa kuwapatia mafunzo ya biashara ya ujasiriamali na wengine 100 wamepatiwa vitendea kazi vya kuendelezea biashara zao. Katika awamu ya pili, Airtel Fursa imeahidi kutumia zaidi ya Sh. bilioni moja ukiwa na lengo la kuwawezesha vijana kwa kuwapatia mbinu mbalimbali za biashara na vifaa vitakavyowawezesha kukuza biashara zao.

Habari Kubwa