Airtel Fursa yainua kikundi cha vijana wajasiriamali Lindi mjini

26Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lindi
Nipashe
Airtel Fursa yainua kikundi cha vijana wajasiriamali Lindi mjini

WAFANYAKAZI wa kampuni ya simu za mkoni ya Airtel mkoani Lindi, wamejumuika na mradi wa kijamii wa kampuni yao wa Airtel Fursa kwa kuwawezesha vijana wajasiriamali wa kikundi cha Sauti ya Jamii kwa kuwainua kibiashara na kuwajengea banda la kisasa la ufugaji wa mbuzi.

Wafanyakazi wa Airtel wakawakabidhi moja ya wajasiliamali wa Dar es Salaam zawadi katika promosheni ya Airtel Fursa.

Aidha, Airtel Fursa imewaongezea mbuzi 44 pamoja na vitendea kazi yakiwamo majembe na rato kwa ajili ya kuanza kilimo.

Vijana hao watano, waliamua kuungana baada ya kupata mafunzo kwenye mradi wa `Kijana Jiajiri' uliokuwa ukiendeshwa na shirika la Restless Development.

Mradi huo ulilenga vijana walio nje ya shule kuwajengea uwezo ili wajiajiri na kupunguza ukosefu wa ajira nchini.

Kikundi cha Sauti ya Jamii kimesajiliwa na halmashauri na kiliomba ardhi serikali za mitaa kwa ajili ya kilimo na kupewa ekari 50.

Hata hivyo, ukosefu wa mtaji ndiyo uliwakwamisha kuanza shughuli za kilimo.

Akizungumza wakati wa ujenzi wa banda hilo la kisasa la mbuzi, Kiongozi wa msafara wa ziara hiyo na Meneja Mauzo Kanda ya Lindi, Edmund Lasway, alisema:

“Airtel tunayo furaha kuona tunaweza kusaidia vijana wenye moyo wa kujiendeleza kama hawa. Kabla ya hapa wamekuwa na mbuzi wapatao 14, lakini hawakupata faida ya kutosha," alisema.

"Ni matumaini yetu kuwa fursa hii itawawezesha kufika mbali kibiashara na kupanua wigo wa biashara yao kwa kupata masoko na kuuza mifugo na kulima mazao yao katika ubora zaidi," aliongeza.

Alitoa wito kwa vijana wengine kujitokeza na kutokata tamaa ya maisha na kuchangamkia fursa kama hizo pale zinapojitokeza.

Kwa upande wake, Mwakilisha wa kikundi cha Sauti ya Jamii, Shabani Kikotokeki, alisema: “Tunawashukuru sana Airtel kwa kutuwezesha kuinua biashara yetu na kutupa nguvu zaidi ya kujiendeleza kibiashara na hata kuwatia moyo vijana wenzetu wanaotuzunguka. Tunategemea kuinua kipato chetu na hata familia zetu, hivyo tunawahimiza vijana wengine hapa nchini kutokata tamaa ya maisha na kuchangamkia fursa hizi zinapojitokeza."

Airtel kupitia huduma zake za jamii, imewafikia vijana zaidi ya 20 kwa kuwapatia vitendea kazi katika msimu huu wa pili wa Airtel Fursa na kwa upande wa mafunzo ya biashara ya ujasiriamali imewafaidisha vijana wapatao 1,000 katika msimu huu wa pili wa Airtel Fursa ambapo lengo ni kuwafikia vijana wengi zaidi.

Habari Kubwa