Ajira 2,000 zaja kiwanda cha PPF

17Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ajira 2,000 zaja kiwanda cha PPF

MFUKO wa Pensheni wa PPF unajenga kiwanda kikubwa cha kuchakata ngozi mkoani Kilimanjaro ambacho kinatarajiwa kutoa jumla ya ajira 1,648 kitakapokamilika mwakani.

Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio.

Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, alisema ujenzi wa kiwanda hicho kipya utakaomilika mwakani utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 54.4.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa na viwanda vidogo vinne, ambavyo ni kiwanda cha kisasa cha kuchakata ngozi, kiwanda cha kuzalisha soli za viatu, kiwanda cha kuzalisha viatu na kiwanda cha kuzalisha bidhaa nyingine za ngozi.

Erio alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki wakati ujumbe wa Serikali ulipotembelea mradi wa ukarabati wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga pamoja na ujenzi wa kiwanda hicho kipya cha bidhaa za ngozi, mjini Moshi.

PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza zimeingia ubia katika kuleta mapinduzi ya viwanda ikiwa ni utekeleza wa azma ya Serikali ya awamu ya tano.

Erio alisema kiwanda hicho kitachakata ngozi kiasi cha futi za mraba milioni 3.75 kwa mwaka, kuzalisha viatu milioni 1.2, jozi 900,000 za soli na bidhaa nyingine za ngozi 48,000 kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo alisema kiwanda kitakapokamilika kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 648 na ajira zisizokuwa za moja kwa moja zaidi ya 1,000.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kiwanda hicho.

Alisema PPF na Jeshi hilo pamoja na sekta nyingine za Hifadhi ya Jamii zimeonyesha dhamira ya dhati ya kuisaidia Serikali kufikia malengo yake ya Tanzania ya Viwanda ifikapo 2025.

Ziara hiyo pia iliwahusisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adolf Mkenda na Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini, Dk. Juma Malewa.

Jenista alisema Mfuko wa PPF, Jeshi la Magereza na sekta ya hifadhi ya jamii kwa ujumla zinafanya kazi kubwa na wameonyesha dhamira ya dhati ya kuisaidia serikali ya awamu ya tano kufikia malengo yake ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Alisema Serikali inaunga mkono juhudi njema zinazochukuliwa na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza za kufikia uchumi wa viwanda.

Mawaziri hao waliutembelea mradi huo ili kujionea kazi nzuri zinazofanywa.

Mhagama alisema uamuzi wa PPF na Magereza kuwekeza kwa pamoja katika kuimarisha kiwanda kilichopo cha viatu na kujenga kiwanda kipya kikubwa cha kisasa cha kuzalisha bidhaa za ngozi ni wa kizalendo, na unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.

Alisema uwekezaji kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, ni uwekezaji ambao utakwenda kuwekeza fedha za wanachama mahali salama, kwa sababu miradi hiyo kabla ya kufanyiwa uwekezaji katika uchumi wa viwanda utafiti unafanyika wa kutosha na kila mradi utakaofanywa utakuwa ni mradi ambao utarudisha gharama na kuleta faida.

“Tumekubaliana hapa kwamba ni lazima wanachama wajue, uwekezaji unaofanywa unafaida gani kwa mfuko, lakini utaleta ongezeko gani la tija katika mfuko unaohusika? Hivyo nataka niwatoe hofu wanachama kuwa fedha zao zipo salama, zinalindwa vizuri,” alisema Waziri Mhagama.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti la Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Profesa Madundo Mtambo alisema shirika hilo limehusishwa katika mradi huo kwa ajili ya kuusimamia.

Alisema hivi sasa kiwanda kidogo kinazalisha viatu jozi 150 kwa siku, ambapo kitakapoboreshwa kitatoa viatu 400 kwa siku na kwamba miradi yote hiyo itaongeza ajira na kuingizia Serikali mapato.