Akaunti ya NMB isiyo na makato ya mwezi yapokewa kwa shangwe

12Feb 2024
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Akaunti ya NMB isiyo na makato ya mwezi yapokewa kwa shangwe

MAELFU ya wananchi wa Wilaya ya Temeke, hususani wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake, mwishoni mwa wiki walifurika katika tamasha la kuhamasisha ufunguaji akaunti nafuu isiyo na makato ya mwezi inayotolewa na Benki ya NMB lililopewa jina la NMB Pesa Day.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto), akimkabidhi zawadi ya bodaboda Agnes Maujundu (katikati), baada ya kushinda shindano la kufungua akaunti ya NMB wakati wa tamasha la kuhamasisha wananchi kufungua akaunti ya NMB Pesa kwa Sh. 1,000 Mbagala Zhakem jijini Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi. PCHA: MPIGAPICHA WETU

Tamasha hilo lilifanyika kwenye Viwanja vya Mbagala Zakhiem, likienda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Weka na Ushinde itakayodumu kwa miezi mitatu, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda.

 

Katika tamasha hilo lililotanguliwa na mbio za taratibu ‘jogging’ na burudani za muziki kutoka kwa wasanii kama Miso Misondo na Wazee wa Makoti, Mr Blue, Dulla Makabila na wengineo, Mapunda alipongeza NMB kwa ubunifu katika kusambaza huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi.

 

Mapunda alisema NMB Pesa inakwenda kuwa chachu ya maisha bora kwa wana Temeke na watanzania kwa ujumla, ambako licha ya ‘jogging,’ wahudhuriaji walipewa elimu na huduma za kifedha, mashindano ya vipaji vya muziki, ambako zawadi mbalimbali zilitolewa na kiongozi huyo kwa washindi.

 

"Tupo hapa kwa ajili ya NMB, ambayo inafanya kitu kikubwa sana leo kwa ustawi wa maisha yetu. Kwa kutuletea NMB Pesa, ambayo kwa Sh. 1,000 tu, unafungua akaunti hata ukiwa na simu ya kitochi, akaunti ambayo itakuwezesha kupata huduma zote za kifedha, ikiwamo mikopo, kutuma, kupokea, kutoa fedha na kulipia bili mbalimbali.

 

"Sasa, mimi niwaombe kitu kimoja wana Mbagala, sisi tupo wengi sana na ‘buku buku’ (1,000/-) zipo nyingi sana miongoni mwenu, changamkieni fursa kwa kufungua akaunti za NMB Pesa ili mjiwekee akiba, lakini mpate kunufaika na huduma za kifedha za benki hii.

 

"Hapa kuna droo nyingi zinaendelea kwa wote wanaofungua akaunti sasa, ambapo watajishindia fedha taslimu, majiko na mitungi ya gesi, baiskeli za tairi tatu ‘guta,’ na zawadi kubwa zaidi ya bodaboda ambayo nitaikabidhi mwishoni mwa tamasha hili. Kwahiyo, changamkieni fursa," alihimiza.

 

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna aliwahakikishia wananchi wa Mbagala na Watanzania kwa ujumla kwamba NMB imewaletea fursa inayokwenda kubadili maisha yao, kupitia NMB Pesa Akaunti, ambayo ni ya kidigitali unayofunguliwa kwa Sh. 1,000 tu, ikiwafikia ikiwa na fursa nyingi.

 

"Fursa ya kwanza inayokuja na akaunti hii ni kuwa unaingia moja kwa moja kwenye huduma jumuishi za kifedha kupitia NMB, watoa huduma wametapakaa kote kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa sehemu ya huduma hii inayokuja chini ya kaulimbiu ya ‘Haachwi Mtu.’

 

"Kupitia NMB Pesa, utakuwa umeingia moja kwa moja katika huduma ya NMB Mkononi, inayokupa wigo mpana wa kujihudumia na kuhudumiwa kibenki bila kuja kwenye matawi ama katika ofisi za benki yetu ambako utafanya miamala na malipo na manunuzi kidigitali.

 

“Pia rekodi zako kipesa kupitia NMB Pesa Akaunti zitakuongezea fursa kwani kubwa kuliko yote utaweza kukopa hadi Sh. 500,000 kupitia Mshiko Fasta, huduma ya mikopo isiyohitaji dhamana yoyote wala kujaza fomu. Hapo vipi, haujabadilisha maisha yako?

 

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, hii kampeni tunayoianza leo, ni kampeni ya Weka Akiba na Ushinde. Kwa hiyo, pamoja kufungua akaunti ya NMB Pesa, lakini tunazindua kampeni ya Weka Akiba na Ushinde, yaani unaweka Sh. 50,000 na unajishindia zawadi mbalimbali,” alisisitiza.

 

Zaipuna alibainisha kwamba kila wiki kutakuwa na droo zitakazozalisha washindi 10 wa watakaojishindia Sh. 500,000 kila mmoja, washindi watano wa kila mwezi watazoa Sh. milioni moja na katika droo ya fainali, mshindi atajinyakulia Sh. milioni 10, washindi wanane wa Sh. milioni tatu, mashine ya kufulia, Tv, friji, bodaboda tano na pikipiki nane za mizigo.

 

"Kwa mantiki hiyo, tunawakaribisha Watanzania wote wajiwekee akiba, lakini wabadilishe maisha na kuboresha biashara zao kupitia akiba na zawadi watakazoshinda,” alisema Zaipuna alipozungumza na maelfu ya waliohudhuria tamasha hilo, lililofungwa kwa Agnes Maujundu kujinyakulia bodaboda.