Amwaga chozi ushahidi kesi ya mauaji ya mkewe

06Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Amwaga chozi ushahidi kesi ya mauaji ya mkewe

MFANYABIASHARA John Thomas (59), jana alimwaga machozi na kwikwi wakati akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji ya mke wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mtuhumiwa Oriana Hamis, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza na Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusikiliza mashahidi wanne wa Jamhuri dhidi ya kesi inayomkabili ya mauaji ya Silvester Paul. PICHA: HELLEN MWANGO

Katika ushahidi wake, alidai kuwa msichana wake wa kazi, Oriana Hamisi, alitoroka nyumbani kwake baada ya mauaji ya mke wake mdogo Silvester Paul siku 23 baada ya kuajiriwa.

Kadhalika amedai kuwa kabla ya kutoroka alimpulizia mtoto wake mchanga dawa ya kuuwa wadudu yenye jina la IT.

Thomas alitoa ushahidi huo huku akishikwa na kwikwi ya kulia jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, iliyopewa mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji chini ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Grace Mwanga na Chesenci Gabiola.

Shahidi huyo alidai kuwa makazi yake ni Vingungutu Kiembembuzi, jijini Dar es Salaam.

Alidai Machi 27, 2014 alikuwa akiishi eneo mtaa wa Miembeni akiwa na familia ya wake wawili, mkubwa Manju Thomas na Silvester (kwa sasa marehemu), watoto wao watatu na msichana wa kazi, Oriana, ambaye alianza kazi Machi 4, mwaka huo.

Alidai kuwa siku hiyo, nusu ya familia iliondoka asubuhi, mke mkubwa aliondoka saa 12:00 na yeye na watoto wawili wanaosoma waliondoka saa 12:30 asubuhi huku wakimwacha mke mdogo na mtoto wake mchanga wa mwaka mmoja na nusu na msichana wa kazi.

"Saa saba mchana niliongea na mke wangu mdogo nikiwa kazini, Kunduchi, lakini ipofika saa 11:00 jioni nilipigiwa simu na aliyekuwa dereva wangu kwamba mtoto amerudi shuleni amegonga geti muda mrefu nimpigie simu mama mdogo amfungulie," alidai kuhu akimwaga machozi na kwikwi kwa kilio.

"Nilimpigia simu mke wangu mdogo hakupokea, nikamjulisha dereva wangu amvushe mtoto ukutani ili akajue ndani kuna nini. Nilipigiwa nikaambiwa kuna tukio kubwa ikanilazimu nirudi nyumbani, nikamkuta mke wangu amelala kwenye dimbwi la damu na ana jeraha juu ya sikio la kushoto. Nilimbeba kumuwahisha hospitalini lakini tuchelewa alishapoteza damu nyingi alifariki dunia" alidai na kuangua kilio.

Alidai kuwa mwili ulihifadhiwa katika chumba cha maiti na aliporejea nyumbani alikuta sebuleni kumetapakaa damu nyingi na shoka likiwa chini limejaa damu.

Alidai kuwa wakiwa pamoja na polisi waliingia chumbani kwa mke mdogo kulikuwa kumevurugika kabatini nguo zote ziko chini, dhahabu zimeibwa, kamera ya video na simu ya mke wake pia havikujulikana vilipo.

Walipomtafuta msichana, majirani walieleza kwamba walimwona akiondoka na bodaboda huku akiwa na mzigo.

" Nikaanza kumtafuta mtoto wangu mchanga tulimkuta amelala ananuka dawa ya kuuwa wadudu naona alitaka kumwua na mtoto wangu," alidai Thomas huku akilia.

Alidai kuwa walilazimika kwenda kwa Dada Amina aliyemletea msichana huyo anaishi Tabata Segerea lakini hawakufanikiwa kumkuta naye alishatoroka wakalazimika kwenda kumkamata mume wake na bibi yake ndipo akajisalimisha polisi.

Hata hivyo, alidai kuwa Amina alipoulizwa kuhusu mahali alipo msichana alikana kufahamu lakini baada ya siku sita kumalizika shughuli za mazishi, Oriana alimpigia simu akidai amepata ajali yuko Tabata lakini tayari kitengo cha mawasiliano cha jeshi la polisi kilinasa mawasiliano hayo na kubaini yuko jijini Arusha.

Baada ya wiki mbili, alidai kuwa walifanikiwa kumkamata Arusha akiwa anafanya kazi kwa mtu mwingine kwa kushirikia na askari polisi wa Arusha na Dar es Salaam.

Alidai kuwa walipompekuwa walikuta na kamera, simu ya marehemu, kadi ya ATM ya benki ya KCB, funguo sita,mkoba na cheti cha hospitali cha mtoto wa marehemu.

Shahidi aliomba mahakama ivipokee kama kielelezo katika kesi hiyo na mahakama ilikubali.

Katika kesi ya msingi, Oriana anadaiwa kuwa Machi 27,2014 alimuua kwa makusudi Silvester kwa kumpiga na shoka kichwani.

Habari Kubwa