Angalizo kali wafanyabiashara mbolea

15Jan 2018
Ibrahim Yassin
Nipashe
Angalizo kali wafanyabiashara mbolea

MKUU wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Claudia Kitta, amewapa angalizo kali wafanyabiashara waliopewa tenda ya kuuza mbolea kwa bei elekezi kuuza kwa kufuata utaratibu uliowekwa wa kuuza kwa bei elekezi badala ya kupandisha bei inayomnyonya mkulima.

MKUU wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Claudia Kitta.

Serikali imebadili mfumo wa ugawaji pembejeo kwa mtindo wa vocha baada ya kuwapo kwa malalamiko mengi ya wakulima kuwa hawanufaiki na mfumo huo ambapo mwaka huu wafanyabiashara watauza kwa bei elekezi ili kila mkulima anunue dukani.

Kufuatia mpango huo, kuna baadhi ya wafanyabiashara walioorodheshwa majina na kampuni zao na kupewa utaratibu huo, ambapo wengi wao wamejiondoa kwa madai mpango huo, unawaminya na kwamba kwa waliokubali wamepewa onyo kali baada ya kuwapo tetesi za kuuza pembejeo kwa bei juu.

Akizungumza jana kwenye mdahalo ulioitishwa na shirika la kiraia la Jitambue Lembuka Tanzania (J.L.T), mwenyekiti wa kamati ya pembejeo wilayani humo, Claudia Kitta, alisema ili kuhakikisha wakulima wanalima kwa manufaa ni lazima maofisa ugani wawafuate wakulima.

Kitta ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, alisema ikibainika wafanyabiashara wanauza pembejeo kwa bei ya kilanguzi kuwachukulia hatua huku akieleza  serikali ya awamu ya tano ni ya viwanda, ili viwanda viweze kuendelea ni lazima wakulima wazalishe mazao mengi.

Aidha, alisema mbali na mkulima kulima mazao mengi, pia aliwataka maofisa kilimo kutokaa maofisini na badala yake waende mashambani kutoa elimu na ushauri kwa wakulima.

Awali akizungumza kwenye mdahalo huo, Asha Kalilobe, mkazi wa kijiji cha Tenende, alisema wakulima wamekuwa hawapati ushari na pia hawawafahamu maofisa ugani wa vijiji wala kata hivyo, alisema viongozi wa kata na halmashauri wanatakiwa kuwasimamia maofisa hao ili kuhakikisha wanafika vijijini.

Stephen Mwangalaba, Diwani wa Ipande, alisema maoni ya wajumbe kwenye mdahalo huo yana mashiko kutokana na umuhimu wa kilimo, na kwamba maofisa ugani hawafahamiki vijijini na hata wao kama madiwani hawashirikishwi kwenye kamati, hivyo maboresho yafanyike.

Simon Mkanya, mkurugenzi wa shirika hilo, alisema wao waliliona hilo, ndiyo maana wameitisha mdahalo huo wakishirikisha viongozi wa vijiji, kata na halmashauri akiwamo mkuu wa wilaya, hivyo majadiliano haya endapo yatafanyiwa kazi, ana uhakika mkulima atanufaika na hata Tanzania ya viwanda itawezekana.

 

 

 

 

Habari Kubwa