Angalizo kwa wakwepa kodi majengo ya serikali

11Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Angalizo kwa wakwepa kodi majengo ya serikali

WAFANYABIASHARA waliopanga katika majengo ya serikali wamepewa angalizo la kulipa kodi kwa wakati mwafaka, vinginevyo wataondolewa katika majengo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Scholastica Kevela.

Angalizo hilo limetolewa na Kampuni ya Udalali ya Yono, ambayo imetangaza operesheni ya kuwaondoa kwenye majengo wafanyabiashara ambao wamepanga kwenye majengo ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao wanakaidi kulipa kodi kwenye Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Scholastica Kevela, wakati akizungumzia operesheni kama hiyo iliyofanyika wiki iliyopita.

Operesheni hiyo ya wiki iliyopita ilihusisha kuziondoa kwenye majengo ya TBA, kampuni ya Air Msae na ya Simon Group, zoezi ambalo Mkurugenzi huyo alisema lilifanikiwa kwa asilimia 100.

“Zoezi la kuindoa Simon Group na Air Msae limefanikiwa kwa asilimia mia na serikali imeshachukua majengo yake na nawaahidi Watanzania kuwa moto huu ambao kampuni imeuwasha hautazimika, huu moto ni endelevu na sasa tunakwenda Moshi na Lindi,” alisema Cholastica.

Aidha, alisema ni vyema watu waliopanga kwenye majengo ya serikali wakalipa mapema kabla ya kuondolewa kwenye orodha badala ya kujidanganya kuwa wanaweza kujificha kwani zoezi hilo ni la nchi nzima.

Habari Kubwa