Angalizo kwa wateja wa Tigo

10Oct 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Angalizo kwa wateja wa Tigo

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Tigo katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani, imewataka wateja wake kuficha nywila zao za Tigo-pesa na kuwa makini pale wanapofanya miamala ya fedha ili kuepusha usumbufu.

Ushauri huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma kwa Wateja, Mwangaza Matotola, wakati wa uzinduzi wa wiki hiyo ambayo itahitimishwa Oktoba 11, mwaka huu, kwa kutoa tuzo kwa mfanyakazi bora wa mwaka ambaye ameonyesha weledi mkubwa katika utoaji wa huduma ikiwa ni njia ya kutoa hamasa kwa wafanyakazi wengine.

Alisema kampuni hiyo inayolenga kuleta mageuzi ya kidijitali katika maisha ya Watanzania, imeimarisha huduma wanazozitoa na kuwezesha wateja kuweza kujihudumia bila kuongea au kuonana na muhudumu moja kwa moja ambapo kwa sasa mteja anaweza kujihudumia mwenyewe pale alipokosea kutuma fedha kwa mtu ambaye sio sahihi na kuirejesha.

“Kwa sasa mteja anaweza kujihudumia mwenyewe hata kama akikosea kutuma pesa kwa mtu ambaye sio sahihi na anaweza kuirudisha mwenyewe bila kupata msaada kutoka kwa mtoa huduma wetu,” alisema Matotola.

Alisema kwa sasa mteja anaweza kupata huduma zake kwa kupitia mitandao ya kijamii Whatsapp, Facebook au kupiga namba 100 ambayo ataweza kuhudumiwa.

Alisisitiza kampuni hiyo kwa sasa inajivunia kuwa na wafanyakazi zaidi 1,000 ambao wanahudumia wateja zaidi ya milioni 11 kwa saa 24, hivyo katika wiki hii wametambua mchango mkubwa kutoka kwa watoa huduma wao wanaoendana na kauli mbiu ya wiki isemayo “Magic of Service” yaani huduma ya maajabu.

Habari Kubwa