Apiga ‘stop’ machinga kutozwa 500/- za usafi

26Mar 2020
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Apiga ‘stop’ machinga kutozwa 500/- za usafi

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni, amepiga marufuku viongozi wa soko la madini la jijini humo, kutoza Sh. 500 wafanyabiashara wadogo wa madini (machinga) kwa ajili ya usafi.

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni, picha mtandao

Akitoa agizo hilo jana alipotembelea soko hilo, Dk. Madeni alisema, kitendo cha kutoza wafanyabiashara hao fedha hizo ni kwenda kinyume na agizo la Rais John Magufuli la kuzuia machinga kutozwa ushuru.

“Mimi nimepata malalamiko toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, kuwa katika soko hili mnatozwa ushuru na Mwenyekiti wa soko hili, Abugasti Mollel, kwa ajili ya usafi, kuanzia sasa ‘stop’ kama usafi nitaagiza kampuni iliyopewa tenda ya kuzoa taka katika jiji hili, ili waje hapa sokoni kila siku kuchukua takataka, sitaki kusikia watu wanatoza fedha,”alisema.
Alisema fedha zinatozwa kwa kutoa risiti za kawaida na siyo za elekroniti (EFDs), jambo ambalo halikubaliki.

Alimuagiza mwenyekiti huyo (Abugasti) kuwa makini na kuifahamu mipango ya baadhi ya wanasiasa ambao wana malengo yao ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) au nje ya chama hicho ya kumuharibia Mkuu wa wilaya aonekane hafai katika kazi, kwa kutoa maelekezo yalio tofauti na maagizo ya Rais Magufuli.

Hata hivyo, alisema kitendo cha kutoza wafanyabiashara hao fedha hizo, ilikuwa amfunge pingu na kumpeleka mahabusu, lakini kwa sababu alikiri kutoza watu fedha hizo kwa maelekezo ya Kamishna wa Madini wa mkoa huo (RMO), Hamisi Kamando, alimsamehe.

Kwa upade wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, alimuagiza Mkurugenzi Dk. Madeni kutembelea soko hilo na maeneo yote yenye malalamiko na machinga kutozwa ushuru na kushughulikia haraka changamoto hiyo.

“Mimi nimepokea malalamiko toka kwa baadhi ya machinga wa soko la madini Arusha, wakilalamika kutozwa Sh. 500 kwa ajili ya usafi wa soko hilo, hiki kitendo ni kinyume na agizo la Rais, sasa naomba mkurugenzi nenda kwenye soko hilo ukapige ‘stop’ uchangishaji wa fedha hizo,” alisema.

Pia aliwaomba machinga hao kuacha kutumika kisiasa na hasa mwaka huu wa uchaguzi mkuu na kuhakikisha wanampa kura mtu aliyehangaika nao.

Akitoa utetezi wake mbele ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo, Mwenyekiti wa soko hilo, Mollel alikiri kutoza Sh. 500 wafanyabiashara hao wadogo wa madini, lakini kwa maelekezo ya RMO.

“Mimi natoza fedha hizi lakini siwezi kutoa maelekezo yoyote sababu msimamizi wa soko hili RMO na ndiyo aliniagiza nichukue fedha hizi, ili tufanye usafi wa soko hili,”alisema.

Kamishna wa Madini Mkoa wa Arusha, Hamisi Kamando alipopigiwa simu na Dk. Madeni kuhusu utozaji huo wa fedha, alikiri kutoza fedha hizo ka ajili ya usafi na ulinzi na kuahidi kutotoza tena.

Habari Kubwa