Apigia debe ufugaji mbegu za chupa

20Mar 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Apigia debe ufugaji mbegu za chupa

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel, ameagiza halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa kutumia mbegu bora zinazozalishwa kituo cha Taifa cha Uhimilishaji Mifugo kwa Njia ya chupa (NAIC) kilichoko Arumeru, mkoani hapa.

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel, picha mtandao

Prof. Ole Gabriel alitoa agizo hilo jana katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, kutokana na mwamko mdogo wa kutumia mbegu hizo.

Alisema ili kuendana na uchumi wa viwanda ni lazima wafugaji wabadilike na kutumia mbegu hizo ili kupata ng'ombe wenye nyama bora, maziwa, ngozi na kwato zitakazokidhi malighafi za viwanda.

Katibu Mkuu huyo alisema kwa kipindi cha mwaka jana, walitoa mafunzo kwa wafugaji 58,000 kwa nchi nzima hali iliyosababisha kuzalisha ndama 10,000 pekee licha ya kituo hicho kuzalisha mbegu 60,000 kwa wiki.

"Idadi ya wagufaji waliopewa elimu ni ndogo na mwitikio wa utumiaji mbegu hizi hauridhishi kwa wafugaji wetu. Kituo kinazalisha mbegu za kutosha kwa mahitaji ya wafugaji wote nchini, hivyo nawaagiza wataalamu wote watoke ofisini waende kwa wafugaji kutoa elimu juu ya utumiaji mbegu hizi," alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kuwataka wafugaji kuondokana na dhana potofu kwamba kutumia mbegu hizo ni kuharibu vizazi vya mifugo jambo ambalo si sahihi.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema hali ya usambazaji wa mbegu hizo kwenye vituo vilivyoko kanda saba nchini hauridhishi kutokana na baadhi ya wataalamu kutotimiza wajibu wao wa utoaji elimu kwa wafugaji.

"Serikali inauza mbegu hizi kwa ruzuku ili wafugaji wasiokuwa na uwezo wamudu gharama ya Sh. 5,000, lakini kuna baadhi ya wataalamu wananunua mbegu hizi na kuziuza kati ya Sh. 15,000 na Sh. 40,000," alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Mjai, Mahmoud Mgimwa, alisema utumiaji wa mbegu hizo utawezesha wafugaji kufuga kwa tija na kupata soko la uhakika la bidhaa za mifugo yao.

"Kikubwa hapa wafugaji wabadilike kutoka kwenye ufugaji wa mazoea na kufuga kisasa kwa kutumia mbegu hizi, tushiriki uzalishaji wa malighafi za viwanda vyetu vinavyoanzishwa kwa wingi nchini," alisema.

Habari Kubwa