Asasi za wanawake zashauri elimu ya mikopo kutolewa kuanzia vijijini

17Jun 2021
Christina Haule
MOROGORO
Nipashe
Asasi za wanawake zashauri elimu ya mikopo kutolewa kuanzia vijijini

ASASI za wanawake mkoani Morogoro zimemshauri Rais Samia Suluhu Hassan, kuwawezesha wanawake kwa kuanza kuwapatia elimu ya kina juu ya mikopo kuanzia ngazi za vijiji jambo ambalo litakasaidia kuondoa ufujaji wa fedha hizo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Asasi ya Wezesha Mabadiliko, Lusako Mwakiluma alipozungumzia kauli aliyoitoa Rais Samia juu ya kuwezesha wanawake kiuchumi wakati akiongea na wawakilishi wa wanawake wa Tanzania jiijini Dodoma.

Amesema yeye akiwa kiongozi wa Asasi ambaye tayari ameshatoa mikopo amebaini uwepo wa wanawake wengi wenye uelewa mdogo juu ya fedha za mikopo na suala zima la kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mwakiluma, amesema wapo wanawake ambao hawaoni sababu ya kukopa na wengine hukopa bila kufanyika malengo waliyokusudia na kuishia kutumbukiza hela za mkopo kwenye manunuzi ya nguo na kwenda kwenye sherehe za wenzao bila kujua watarejesha nini huku wengine wakikopa sehemu moja na kupeleka kwenye mkopo mwingine badala ya kuzungusha.

"Mimi pia niliwahi kukopesha na kuingia hasara ya Sh. milioni 10, nilikopesha wanawake wa kata ya Uwanja wa Taifa ambao hawakuonesha ushirikiano wowote wa kulipa mpaka leo, lakini yote hiyo ni matokeo ya uelewa mdogo" amesema.

Hivyo amesema ikiwa wanawake wote watapewa elimu ya kujitambua itakayosaidia hata Serikali itapoanza kuwawezesha kiuchumi kuona umuhimu wa fedha hizo na kuzifanyia miradi endelevu kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya kijamii ya My Health Foundation, Herieth Mkaanga amewaasa wanawake kujenga tabia za uaminifu kwa kurejesha pindi wanapopewa mikopo ili kufanya na wenzao kupatiwa mikopo baadae.

Hivyo Mkaanga alimshkuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi jambo alilosema litafanikiwa endapo wanawake wenyewe wataonesha ushirikiano. 

Mmoja wa wanawake wa Manispaa ya Morogoro Getruda Raphael alimshkuru Rais Samia kwa moyo wake wa kutaka kuwawezesha ambapo aliahidi kuitumia vizuri fursa hiyo katika kujiletea maendeleo. 

Habari Kubwa