Asiyetoa risiti kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi

23Apr 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Asiyetoa risiti kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema itamchukulia hatua za kisheria ikiwamo kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi mfanyabiashara yeyote ambaye atabainika hatoi risiti za manunuzi kwa mteja.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani, Abdul Zuberi, katika kikao cha watumishi wa TRA na wafanyabiashara kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mbeya.

 

Zuberi alisema baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu kwenye biashara zao na badala yake huiibia serikali kwa kutotoa risiti za manunuzi wa wateja wao.

 

Alisema kitendo hicho sio cha kizalendo bali kinalengo la kuiibia serikali mapato na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

 

Alitoa rai kwa wafanyabiashhara kote nchini kufanya biashara zao kwa kufuata kanuni na taratibu na kuwa waaminifu katika ulipaji wa kodi ili fedha zinazokusanywa zitumike kwenye shughuli za maendeleo.

 

“Kama kuna mfanyabiashara yeyote ambaye anauza bidhaa zake bila kutoa risiti aache mara moja ukikamatwa utakuwa na kesi ya kujibu kuhusu uhujumu uchumi, nawashauri zingatie kanuni na sheria zilizowekwa kwenye kodi ili mfanye biashara zenu kwa uhuru,” alisema Zuberi.

 

Katika hatua nyingine Zuberi aliwashauri wafanyabiashara kutokuwa wepesi wa kulipa kodi kwa watu wanaodai wanakusanya kodi kwenye maeneo ya biashara zao na badala yake wawe makini na ikiwezekana kufika katika ofisi za TRA kulipa.

 

Alisema baadhi ya watumishi wa serikali sio waaminifu, hutumia mwamvuli wa TRA kuwaibia wafanyabiashara, hivyo aliwataka kuwa makini kulipa kodi.

 

“Mfanyabiashara kama unamashaka na mtumishi anayekusanya kodi usimpe badala yake fika kwenye ofisi za mamlaka ndipo utoe na uhakikishe unapewa risiti,” alisisitiza Zuberi.

 

Baadhi ya wafanyabiashara akiwamo, Peter Mwalongo, aliiomba TRA kuangalia upya gharama za kodi ya majengo ambayo inadaiwa kuwaumiza baadhi ya wananchi.