Askofu Shoo aomba uwekezaji SMMUCo

26Mar 2020
Godfrey Mushi
Hai
Nipashe
Askofu Shoo aomba uwekezaji SMMUCo

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo, amewataka waumini wa kanisa hilo na watu wenye nguvu kiuchumi kutosita kuongeza nguvu katika uwekezaji wa majengo ya kisasa na miundombinu ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Askofu Stefano Moshi (SMMUCo).

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo, picha mtandao

Wito huo wa Dk. Shoo, unalenga zaidi kukiboresha chuo hicho katika suala la majengo, miundo mbinu na rasilimali watu ili kutimiza matakwa ya Kamisheni ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) ya vyuo kujitanua na kuwa na hadhi ya kimataifa.

Alikuwa akizungumza jana na viongozi wa Usharika wa Lyamungo Sinde uliopo Jimbo la Hai la Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, baada ya kuchangisha kiasi cha Sh. milioni 2.7 za uboreshaji wa chuo hicho.

“Ni lazima kama kanisa na Dayosisi ya Kaskazini, tujitahidi sana mwaka huu kukiweka chuo chetu katika hadhi ya kisasa ili kukitangaza zaidi kitaifa na kimataifa, niwaombe sana muendelee kuchangia hasa ndugu zangu mliojaliwa uwezo wa kiuchumi msirudi nyuma kutusaidia katika jambo hili,”alisema Dk. Shoo.

Desemba 25 mwaka jana, Askofu Dk. Shoo, alitangaza uamuzi wa Dayosisi hiyo wa kusimamishwa kwa michango ya mingine ya miradi ya kikanisa kuanzia mwaka 2020 katika Dayosisi ya Kaskazini ili kuruhusu fedha zitakazochangwa zitumike kukiboresha SMMCo.

Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alitangaza neema nyingine kwa waumini wake, baada ya kuridhia kuongeza ufadhili wa masomo kutoka wanafunzi watatu hadi sita kutoka kwenye sharika zake kuanzia mwaka wa masomo 2020/21.

Dayosisi hiyo ilitangaza mwanzoni mwa mwezi huu kuanza kutoa ufadhili huo wa masomo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Stephano Moshi (SMMUCo) katika ngazi ya cheti na stashada.

Kozi zilizopata ufadhili huo ni fani za Maendeleo ya Jamii, Uhasibu, Uandishi wa Habari na Usimamizi wa Biashara.

Habari Kubwa