Ataka kinamama kulindwa na zebaki

08Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Ataka kinamama kulindwa na zebaki

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Kabula Shitobelo, ameitaka serikali kuwakinga kinamama wanaochenjua dhahabu na sumu ya zebaki kwa kuwa ina madhara makubwa kiafya.

Akiuliza swali bungeni jana, Shitobelo alihoji serikali ina mpango gani wa kuwakinga kinamama hao.

Katika majibu ya Wizara ya Madini, ilisema mpango wa serikali katika kuwakinga kinamama wanaochenjua dhahabu kwa kutumia kemikali ya zebaki ni kuendelea kutoa elimu ya uchimbaji na uchenjuaji salama wa madini pamoja na madhara ya kemikali hiyo kwa wachimbaji wadogo.

Ilisema elimu hiyo inatolewa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Pia ilisema katika utekelezaji wa mpango huo, serikali kupitia Wizara ya Madini imejenga vituo vitatu vya mfano vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika maeneo ya Itumbi (Chunya), Lwamgasa (Geita) na Katente (Bukombe) ambayo yameonekana kuwa na wachimbaji wadogo wengi zaidi.

Ilibainisha kuwa teknolojia ya uchenjuaji inayotumika katika vituo hivyo ni Carbon –in –Pulp (CIP) ikiwa ni mbadala wa matumizi ya kemikali ya zebaki.

Hata hivyo, ilisema zipo kampuni za uchimbaji mdogo ambazo zimeanza kuchenjua dhahabu kwa kutumia teknolojia ya ‘shaking table’ ambayo haitumii zebaki wala kemikali yoyote.

Ilisema teknolojia hiyo wizara inaendelea kuifanyia majaribio ili kuona tija yake kabla ya kuanza kuitumia kwa wachimbaji wote hasa wadogo.