Ataka utafiti nyavu za kuvulia dagaa

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Ataka utafiti nyavu za kuvulia dagaa

MBUNGE wa Ukerewe (CCM), Joseph Mkundi, ameitaka serikali kufanya utafiti utakaoainisha matumizi ya nyavu kutegemea aina ya dagaa wanaopatikana kwenye ziwa husika.

Akiuliza swali bungeni jana, Mkundi alihoji kwa nini serikali isifanye utafiti huo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) hufanya utafiti mara kwa mara  ili kubaini athari za matumizi ya zana na mbinu mbalimbali za uvuvi kwa rasilimali za uvuvi na kisha kuishauri serikali.

Alisema wizara yake ina jukumu la kulinda, kuhifadhi, kuendeleza na kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi hapa nchini zinavunwa kwa busara ili ziwe endelevu kwa manufaa ya kuchumi, kijamii na taifa kwa ujumla.

Naibu huyo alisema kifungu cha 66(1) (k) cha kanuni za uvuvi za mwaka 2009, nyavu za dagaa zenye ukubwa wa macho chini ya milimita nane zimekatazwa kutumika kwa uvuvi katika maji baridi ikiwamo Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Aidha, alisema utafiti uliofanyika katika Ziwa Victoria, unaonyesha kuwa kuna aina moja tu ya dagaa anayejulikana kwa jina la kitaalamu ‘Restrineobola argentea’.

Alisema utafiti pia unaonyesha nyavu zenye macho kuanzia milimita nane zikitumika kuvua dagaa wa Ziwa Victoria zitavua waliopevuka na matumizi ya nyavu zenye matundu chini ya milimita nane zikitumika zitavua dagaa wachanga na hiyo itaathiri uvuvi wa dagaa katika Ziwa Victoria.

"Sheria ya Uvuvi na Kanuni zake imezingatia aina ya dagaa katika maji baridi (Maziwa) na maji ya bahari," alisema.

Habari Kubwa