AUWSA yatakiwa kuwa na mapokezi bora kwa wateja

15Jan 2022
Daniel Sabuni
Arusha
Nipashe
AUWSA yatakiwa kuwa na mapokezi bora kwa wateja

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda, ameipa somo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), kuhakikisha katika maandalizi ya mkataba wa huduma kwa mteja, jambo la kwanza liwe ni kuwapo kwa mapokezi mazuri kwa wananchi wanapofika kwenye ofisi zao kupata huduma.

Mtanda aliyasema hayo jana, wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa maji kilichokutana pamoja na mambo mengine, kujadili ushiriki wao katika ukusanyaji wa maoni juu ya maandalizi ya mkataba wa huduma kwa mteja.

Alisema kuwa AUWSA wakitaka kutoa huduma bora ni lazima waanze na mapokezi mazuri kwa mteja anapofika kutaka kuhudumiwa.

“Muwe na ushirikiano na muda na wateja, kwa sababu mapokezi ni kitu muhimu kinachoashiria uhai wa ofisi. Mapokezi humfanya mteja kuridhika na kuwa na uhuru wa kujieleza, lakini pia muwasikilize kwa umakini na kuwahudumia kwa upendo,” alisema Mtanda.

Aidha, alifafanua kuwa wanaopewa huduma ni wananchi, hivyo wawape kipaumbele kwa vile wao ndiyo wadau wakubwa, na ndiyo wanaoiweka serikali madarakani.

Pia, aliitaka mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala yote ya majisafi na maji taka na maendeleo ya mradi mkubwa wa maji, unaotekelezwa na serikali pamoja na Benki ya Dunia (WB), wenye thamani ya Sh. bilioni 520.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na mkataba huo, Ofisa Uhusiano wa AUWSA, Masoud Katiba, alisema mamlaka hiyo imeandaa mkataba wa huduma kwa mteja, kwa madhumuni ya kuwafahamisha wateja na wakazi wa maeneo yote yanayohudumiwa na AUWSA mambo muhimu kuhusiana na huduma wanazozitoa na jinsi wanavyofanya kazi.

Alisisitiza kuwa mkataba huo ni mwongozo wa utendaji kazi na kilimo cha mafanikio ya huduma zinazotolewa, kwa kuwa unalenga kuboresha utendaji kazi, kuongeza uwajibikaji.

Yamo pia masuala ya kuongeza uwazi katika kuwahudumia wateja na pia unaeleza namna ambavyo mteja atatoa mrejesho na namna ya kuwasilisha malalamiko iwapo hataridhika na huduma zinazotolewa.

Habari Kubwa