Awaamsha maofisa ugani

15Jan 2018
Dege Masoli
Nipashe
Awaamsha maofisa ugani

MBUNGE wa Lushoto, Shaban Shekilindi, amewataka maofisa ugani kuleta mabadiliko ya kilimo kuwaelekeza wakulima namna wanavyoweza kujinasua kupitia ardhi.

MBUNGE wa Lushoto, Shaban Shekilindi.

Shekilindi maarufu kwa jina la ‘Bosnia’,  aliyasema hayo wakati wa ziara ya kuwatembelea wananchi katika vijiji  kuhamasisha shughuli za uzalishaji na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi.

Aliwataka maofisa ugani kuamsha kilimo kwa kwenda kwa wakulima na kuwapa elimu ya namna ya kulima kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao bora na ya kutosha, hivyo kujiletea tija wao na taifa kwa ujumla.

Akihutubia wananchi  katika kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola, Shekilindi alilaani baadhi ya maofisa ugani wanaokaa  maofisini na kusubiri wakulima kwamba wamekuwa kizingiti  kwao cha kujikomboa kupitia kilimo na kuwataka kuacha tabia hiyo na kutoka maofisini.

“Ndugu zangu maofisa ugani nawashaurini nendeni kwa wakulima, wananchi wanaojishughulisha na kilimo wengi hawana uelewa wa namna ya matumizi bora ya ardhi na kulima kisasa...  jambo hili limekuwa likichangiakurudisha maendeleo yao nyuma,” alisema Shekilindi.

Aliwataka  watambue kuwa  ni jukumu lao kubwa la kuhakisha wanakwenda kwa wananchi kuwaelimisha juu ya kulima kilimo chenye tija kwani hiyo itawasaidia  kupata mafanikio na kwamba kutowatembelea na kukaa maofisini ni dhuluma na hujuma kwa nchi.

“Kwani elimu ambayo mnaweza kuitoa inaweza kuwa chachu ya wakulima kulima mazao mazuri yatakayokuwa ya ushindani na soko la kisasa, hivyo jambo hilo ni muhimu sana,” alisema.

Aidha, aliwahimiza wakulima na wananchi kwa ujumla kujiandaa na ujio wa miradi  mbalimbali  mikubwa  inayoletwa mkoani Tanga ukiwamo wa bomba la mafuta na kwamba waitumie kama fursa ya wao kujinufaisha, ili wasiwe wasindikizaji.

Habari Kubwa