Awamu ya tano yaipaisha Pwani kiviwanda

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
PWANI
Nipashe
Awamu ya tano yaipaisha Pwani kiviwanda

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, ameeleza mafanikio ya mkoa huo ndani ya miaka mitano kuhamasisha ujenzi jumla ya viwanda 1,236 kulinganisha na mwaka 2015 ambapo kulikuwa na viwanda 300.

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Ameeleza hayo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa linaloratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) kujadili mafanikio na kuibua mapendekezo ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ndani ya mkoa na nchi kwa ujumla.

“Kuna jumla ya viwanda vikubwa 68, viwanda vya kati 112, vidogo 168 na viwanda vidogo sana 888 jambo ambalo linadhihirisha mafanikio makubwa ndani ya mkoa katika kipindi cha uongozi wa awamu ya tano,” alisema Ndikilo.

Aliongezea mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kuhakikisha malengo ya mkoa yanatekelezeka kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Mhandisi Ndikilo pia alielezea kuwa mkoa uliandaa maonyesho ya bidhaa kwa mwaka 2018/19 kwa lengo la kutambulisha bidhaa na kukuza soko la ndani na nje ya nchi jambo ambalo lilipokelewa vizuri na Watanzania wote.

“Rai yangu kwa Watanzania ni kuwa wazalendo kwa kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, jambo litakalosaidia kukuza ajira na pato la taifa kuongezeka,” alisema.

Alisema mkoa umeweza kutengeneza ajira kwa zaidi ya 20% kwa mwaka 2020 ukilinganisha na 5% kwa mwaka 2015/16, ambapo zaidi ya Watanzania 200,000 wamepata ajira nchini.

“Mafanikio haya yametokana na dhamira ya dhati ya Rais John Magufuli ya kutaka nchi kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025,” alisema Ndikilo.

Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk. Godwill Wanga, alisema serikali imeboresha mazingira ya biashara na kupelekea idadi ya wawekezaji kuongezeka katika kipindi cha miaka mitano.

“Uwekezaji wa nje umeongezeka kutoka Dola za Marekali milioni 850 mpaka kufikia Dola bilioni 1.1 jambo ambalo limeiongezea nchi fedha za kigeni na kufanya pato la taifa kuhimalika,” alisema Dk.Wanga.

Aidha alieleza kuwa kupungua kwa riba za mikopo kwa mwaka kutoka asilimia 20 mpaka kufikia asilimia 14 na kuongezeka kwa mikopo benki na kufikia asilimia 7 inaonyesha namna ambavyo serikali imeendelea kuboresha mazingira na kufanya uchumi kukua.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Pwani, Jovita Mavoa, aliishukuru serikali kwa kutenga fungu ndani ya halmashauri iliwezesha kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwafanya kufungua biashara zao na kuwafanya waweze kudumu maisha.

Masudi Ngingite mwenyeketi wa waendesha pikipiki Pwani, alisema wanaendesha shughuli zao kwa ufanisi kutokana na ushirikiano uliopo kati ya serikali na kundi hilo kwa kulifanya liendelee na shughuli za kuwaingizia kipato.

Habari Kubwa