Bahi yapokea mbegu bora za alizeti

26Nov 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Bahi yapokea mbegu bora za alizeti

WILAYA ya Bahi imepokea tani 28 za mbegu bora za alizeti huku kila kata ikipatiwa tani moja kwa ajili ya kuwauzia wakulima wa zao hilo ili wafanye kilimo chenye tija na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yalibainishwa jana na ofisa kilimo wa Kata ya Kigwe Wilaya ya Bahim, Abdallah Mdiliko, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuinua kilimo cha alizeti. 

Alisema wakulima wamechangamkia mbegu ya alizeti iliyotolewa na serikali kwa bei ya ruzuku, hali inayomaanisha kutakuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa zao hilo katika Wilaya ya Bahi kama serikali ilivyokusudia kufanya kilimo hicho. 

Aliema mbegu hizo zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku ya Sh. 7,000 kwa kilo mbili na mpaka sasa asilimia 75 ya mbegu zimeshanunuliwa na wakulima.

Alisema wamejipanga kuhakikisha wakulima wanatumia mvua zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni kwa kupanda mazao yanayostawi katika maeneo yao na kupanda katika maeneo yaliyotifuliwa.

Kadhalika, Mdiliko alisema mvua zimekaribia kuanza na wakulima wameanza kuberega mashamba na wengine tayari wamelima wanasubiri tu mvua zinyeshe ili wapande.

Vilevile, alisema wamekuwa wakisisitiza sana kwa wakulima, kutifua mashamba ili kufanya maji yasitembee shambani na kwenda kusababisha maporomoko.

Hata hivyo, alisema kuwa watu wengi hawalimi mpaka chini bali wanalima kwa kuparua na mvua inaponyesha maji yanapita na kuacha udongo ukiwa mkavu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwe, Jeremiah Sobayii, alisema  wanaishukuru serikali  kwa kutoa mbegu za ruzuku za alizeti ambalo ni zao la kimkakati  hali itakayowezesha watu wa kipato cha chini kumudu bei.
 
Alisema kata hiyo yenye wakazi 3,900 shughuli kubwa ni kilimo na ufugaji hivyo mbegu hizo zitasaidia kuwainua wakazi wa eneo hilo.

Habari Kubwa