Balozi Iddi atamani eneo la kudumu kufanyia maonyesho

16Jan 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Balozi Iddi atamani eneo la kudumu kufanyia maonyesho

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na eneo maalum kwa ajili ya maonyesho ya tamasha la biashara ili kukidhi mahitaji halisi ya washiriki wa maonyesho hayo katika mazingira yote ya hali ya hewa.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, picha mtandao

Alisema utaratibu wa kukodi mahema au ujenzi wa mabanda kwa ajili ya shughuli hiyo unaofanyika kila mwaka unagharimu fedha nyingi.

Balozi Iddi alisema hayo wakati akizungumza na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, alipofanya ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali kwenye tamasha la tano la biashara kusherehekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema serikali kuu tayari imeshaamua kuwapo kwa mpango huo na kinachohitajika kwa sasa ni wizara na taasisi zinazohusika na masuala ya maonyesho kulifanyia kazi suala hilo.

Balozi Iddi alisema watendaji wa taasisi hizo wanapaswa kusoma kwa kufuatilia taasisi za wenzao zilizo Tanzania Bara ambazo tayari zimeshapiga hatua kubwa ya maendeleo katika masuala ya matamasha na maonyesho mbalimbali.

“Yapo maonyesho ya biashara Dar es Salaam, Morogoro na hata Dodoma ambayo tumekuwa tukiyashuhudia na wakati mwingine hupata nafasi ya kualikwa kama wageni rasmi. Hivyo si vibaya kwenu kuiga mifano hiyo,” alisema Balozi Iddi.

Katika matembezi hayo Balozi Iddi, alivutiwa na bidhaa tofauti zinazozalishwa na wajasiriamali wa Zanzibar, Tanzania Bara pamoja na baadhi ya wale wa nchi za Afrika ya Mashariki kama Uganda, Kenya,
Rwanda na Burundi.

Naye Mkurugenzi wa Biashara na Masoko Zanzibar, Khamis Ahmada Shauri, alisema jumla ya taasisi 290 zimeshiriki maonyesho hayo ikiwa ni ongezeko la taasisi 71 ikilinganishwa na taasisi 250 za mwaka jana.

Shauri alieleza kuwa katika mgawanyo huo taasisi za serikali mwaka huu zimefikia 55, zile zilizotoka Tanzania Bara zilikuwa 44, Rwanda 3, Kenya 3, Uganda 3, Burundi 1 na Misri 2.

Alisema uongozi unaosimamia tamasha hilo umelazimika kuwapanga washiriki wa maonyesho hayo katika maeneo finyu kutokana na ongezeko kubwa la taasisi zilizothibitisha kushiriki maonyesho hayo.

Alieleza kwamba Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko inaendelea kufarajika na ushiriki wa taasisi hizo unaokwenda sambamba na hamasa ya wananchi wanaopendelea na kujitokeza kutembelea maonyesho hayo hasa wakati wa jioni na usiku.

Habari Kubwa